HALI ndani
ya klabu ya soka ya Simba imezidi kuwa mbaya
baada ya mjumbe wa kamati ya Utendaji na Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya Zacharia
Hans Poppe kujiuzulu.
Hatua hiyo
inafuatia timu hiyo kufanya vibaya katika michezo yake ya ligi kuu ya Vodacom,
pamoja na kutolewa katika raundi ya kwanza kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na
Recreativo do Libolo ya Angola
wiki iliyopita kwa jumla ya mabao 5-0.
Habari za
uhakika kutoka ndani ya klabu ya Simba zinaeleza kwamba, mara baada ya kutolewa
kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Poppe
ambaye pia ni mwenyekiti wa kundi la marafiki wa Simba ‘Friends of Simba’ alisema
atatoa uamuzi mzito.
Kiongozi
mmoja wa Simba amesema leo kwamba, Poppe alishindwa hata kuhudhuria kikao cha
kamati ya utendaji ya Simba pamoja na wadhamini wa klabu hiyo kilichofanyika
jana usiku kwa ajili ya kujadili ripoti ya timu hiyo baada ya mchezo wake wa
Libolo.
Alisema
Poppe hakutoa sababu zozote za kutohudhuria kikao hicho ambacho baada ya
kupokea ripoti ya kamati ya utendaji kiliijadili na kutoa uamuzi wake.
Poppe ambaye
tayari ameshawasilisha barua ya kujiuzulu kwake jana kwa uongozi wa Simba kwa
akidai kusikitisha na sintofahamu inayoendelea ndani ya klabu hiyo, hivyo
kuamua kujiweka kamndo na kubaki kuwa mwanachama mwaminifu wa klabu hiyo yenye
maskani yake mitaa ya Msimbazi na Twiga.
Mwandishi
wa habari hizi alipomtafuta Poppe kwa ajili ya kuthibitisha taarifa hizi simu
yake iliita bila majibu, huku Katibu wa Simba Evodius Mtawala naye simu yake
iliita bila kupokelewa.
Hivi
karibuni hali ndani ya klabu ya Simba imezidi kuwa ‘tete’ ambapo kumekuwepo na shinikizo la wanachama wa
klabu hiyo kumtaka mwenyekiti wa klabu hiyo, Alhajj Ismail Aden kumtaka
ajiuzulu kwa madai ya kushindwa kuiongoza vema klabu hiyo.
Hata hivyo
Rage amekuwa akikwepa shinikizo hilo kwa madai kwamba wanaocheza ni wachezaji
si viongozi na kwamba hawezi kujiuzulu kwa ajili ya shinikizo la watu wachache
na kama atafikia uamuzi wa kufanya hivyo, atatangaza kwenye mkutano wa wanachama.
Aidha, kuna
taarifa zinabainisha kuwa, kufanya vibaya kwa Simba katika michezo yake
kunatokana na mgomo bairidi unaofanywa na wachezaji wa timu hiyo ambao
wanapinga kubaguliwa na makocha wa timu hiyo pamoja na baadhi ya viongozi.
Simba
ambayo kwa sasa inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 31 imeshauweka rehani
ubingwa wake ambapo sasa Yanga inayoongoza ligi hiyo kwa pointi 42 na Azam Fc inayoshika nafasi ya
pili ikiwa na pointi 36 ndizo
zinazochuana katika kuwania ubingwa wa ligi hiyo.
Comments
Post a Comment