SAMATTA, ULIMWENGU KUJIUNGA NA STARS J'4


WAKATI timu ya soka ya Taifa ‘Taifa Stars’ inaingia kambini kesho kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wake dhidi ya Morocco , nyota wa timu hiyo Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta ambao wanakipiga katika klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wanatarajiwa kujiunga na kambi hiyo Jumanne. 
Stars inayonolewa na Kim Poulsen akisaidiwa na Mzalendo Sylvester Marsh itakwaana na Morocco Machi 24 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa katika mechi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil .
 Ofisa habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Boniface Wambura alisema kwamba, Ulimwengu na Samatta watakuwa wakiitumikia timu yao wikiendi hii katika mechi ya ligi ya mabingwa Afrika ambapo watakuwa nchini Botswana kucheza na timu ya huko.

Alisema wachezaji hao ambao watatua jumanne usiku kwa ndege ya Shirika la Kenya (KQ) wakitokea Nairobi , Kenya , watalazimika kupitia huko kutokana na kutokuwa na usafiri wa moja kwa moja wa kutokea Botswana .

Wambura aliongeza, ukiacha Ulimwengu na Samatta, wachezaji wa Azam Fc walioko nchini Liberia kwa ajili ya mcchezo wao wa kombe la Shirikisho nao watajiunga kambini Jumanne mara baada ya kurejea nchini nchini siku hiyo, huku pia wachezaji wa timu nyingine za Ligi Kuu ambao timu zao zitakuwa na mechi leo za ligi hiyo watajiunga na kambi hiyo mara baada ya kuzitumikia timu zao.

Stars ambayo inayodhaminiwa na kampuni ya Bia Tanzania kupitia bia ya Kilimanjaro itaingia kambini kwenye hoteli ya Tansoma, inaundwa na  makipa Juma Kaseja kutoka Simba ambaye pia ndiye nahodha wa Stars, Aishi Manula (Azam), Hussein Shariff (Mtibwa Sugar) na Mwadini Ally (Azam). Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Erasto Nyoni (Azam), Issa Rashid (Mtibwa Sugar), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Nassoro Masoud Cholo (Simba) na Shomari Kapombe (Simba). 
Viungo ni Salum Abubakar (Azam), Athuman Idd (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Khamis Mcha (Azam), Frank Domayo (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba) na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), huku Washambuliaji ni John Bocco (Azam), Mbwana Mrisho Ngasa (Simba), Simon Msuva (Yanga), na Ulimwengu.

Comments