RUVU SHOOTING YAPANIA KUVUNJA MWIKO WA YANGA KESHO


TIMU ya soka ya Ruvu Shooting imesema ipo tayari kwa mchezo wake wa ligi kuu bara dhidi ya vinara wa ligi hiyo, Yanga utakaopigwa kesho kwenye dimba la Taifa jijini dar es salaam.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, ofisa habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire alisema kwamba timu hiyo inayonolewa na makocha Boniface Mkwasa akisaidiwa na seleman Mtungwe imedhamiria kushinda mchezo huo ili kujiweka katika mazingira ya kuwania ubingwa.
Alisema Ruvu Shooting haiidharau yanga inayoshikilia usukani wa ligi hiyo lakini uwezo wa kusakata kabumbu walionao wachezaji wake unawapa kujiamini na uhakika wa kushinda mchezo huo.
“Tumejipanga vema ili kuweza kushinda mchezo huo, tunafahamu kutakuwa na ushindani wa hali ya juu kwani Yanga ni timu nzuri pia lakini dhamira ya kuiondoka na pointi tatu ipo palepale,”alisema Bwire
Bwire aliongeza kuwa wanataka kuwadhihirishia Watanzania kwamba soka la Tanzania si la Yanga na Simba, bali zipo timu zenye uwezo wa kucheza zaidi yao hususani Ruvu Shooting pale itakapoibukiza mabao ya kutosha Yanga katika mchezo wa kesho.
Aliongeza kuwa pamoja na tambo za ‘Wazee hao wa Uturuki’ kwa kutofungwa tangu waliporejea kutoka Uturuki kuweka kambi ya maandalizi na kudai hawatofungwa na timu yoyoyote, wanataka kuanza kuuvunja mwiko wao huo  na matokeo yao kuishia kuitwa ‘Wapiga debe wa manzese’.
Aidha, Bwire aliomba mwamuzi wa mchezo huo kuchezesha kwa kufuata sheria 17 za soka na mshindi apatikane kwa uwezo wa uwanjani na si kubebwa.
“Nawaomba mashabiki kujitokeza jkwa wingi uwanjani hususani mashabiki wa Simba watakaofarijika na matokeo hayo kuja  kushuhudia maarifa ya sisimizi kumuua tembo, “alisema
Katika hatua nyingine, Bwire alisema wameandika barua kwa Shirikisho la Soka tanzania (TFF) kuomba kuvaa vitambaa vyeusi kwenye mkono wa kushoto pamoja na kusimama dakika moja kabla ya mchezo kwa ajili ya maombolezio ya kifo cha mlezi wao Luteni Simon Thomas.
Bwire alisema Thomas aliseyerkuwa mlezi wa kikosi cha 832 Ruvu JKT alifariki juzi akiwa njiani kwenda hospitali na leo mwili wake utasafirishwa kwenda kwao Musoma kwa mazishi.

Comments