RHINO, KANEMBWA ZASAKA TIKETI VPL


KINDUMBWENDUMBWE cha Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kinaendelea kesho (Machi 9 mwaka huu) katika makundi yote matatu, lakini macho na masikio ya washabiki wa mpira wa miguu yakiwa kwenye mechi za Rhino Rangers ya Tabora na Kanembwa JKT ya Kigoma. 
Timu hizo ndizo ziko katika nafasi nzuri ya kupata tiketi ya kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao kutoka kundi hilo la C. Tayari Mbeya City ya Mbeya na Ashanti United ya Dar es Salaam zimeshapata tiketi za kucheza VPL msimu ujao kutoka kundi A na B. 
Rhino Rangers itaikaribisha Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, wakati Kanembwa JKT itakuwa mgeni wa Pamba kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. 
Mechi nyingine za kundi C ni Mwadui vs Polisi Tabora (Kambarage, Shinyanga), na Morani vs Polisi Mara (Kiteto, Manyara). Mechi za kundi A ni Majimaji vs JKT Mlale (Majimaji, Songea), Mkamba Rangers vs Mbeya City (Sokoine, Mbeya) na Polisi Iringa vs Burkina Faso (Samora, Iringa).
 Mshikeshike ya kundi B ni Ndanda vs Ashanti United (Nangwanda Sijaona, Mtwara), Villa Squad vs Green Warriors (Karume, Dar es Salaam), Polisi Dar vs Transit Camp (Mabatini, Mlandizi) wakati Tessema na Moro United zitacheza Machi 10 mwaka huu Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.