RAGE AKATA TAMAA UBINGWA MSIMBAZI




MWENYEKITI wa klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, Ismail Aden Rage, amekiri nafasi ya kikosi chake kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara ni finyu hasa kutokana na aina ya matokeo mabovu inayovuna katika mfululizo wa ligi hiyo.
Rage aliyasema hayo mara baada ya Wekundu wa Msimbazi Simba kukubali kichapo cha ugenini cha bao 1-0 kutoka kwa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba juzi, matokeo yaliyozidi kuididimiza timu hiyo, wakati alipokuwa akihojiwa na kipindi cha Spoti Leo cha Radio One.
Watetezi hao wameendelea kubaki katika nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi hiyo, wakiwa na pointi 34, sita nyuma ya Azam FC inayoshika nafasi ya pili, huku Yanga ikiongoza kwa pointi 48.
Rage katika kile kilichoonekana kama ‘kukubali matokeo’, alisema sio lazima kila mwaka bingwa wa ligi hiyo akawa Simba, hasa kutokana na ushindani mkubwa uliopo miongoni mwa timu shiriki 14 za Tanzania Bara.
Kama tunataka kuchukua ubingwa kila mwaka, basi tungeunda ligi yetu ambayo ingekuwa na timu tano za Simba ili kila mwaka tuwe mabingwa sisi wenyewe. Lakini hatuwezi kutwaa ubingwa kila mwaka kwa kuwa kuna timu nyingi zinazouwania,” alisema Rage.
Katika msisitizo wake, Rage alisema kufuatia matokeo hayo ya Simba hawezi kujiuzulu, kwa kuwa aliahidi kuijenga Simba imara ambapo alisema atashirikiana na viongozi wenzake katika kuhakikisha hali inakuwa shwari na timu inafanya vizuri tena.
“Mimi si kocha wala sio mchezaji. Kwani mimi ni beki? Kwa hiyo mkiniuliza habari za matokeo mabovu siwezi kuwaambia lolote, zaidi ya ukweli kuwa ni hali ya mchezo ambao una matokeo ya kushinda, kupoteza au sare,” alisisitiza Rage.
Aidha alibainisha kuwa anajipanga kuweka mambo sawa kuhusu hatima ya mgogoro baina yake na baadhi ya wanachama, ambao baadhi yao hivi karibuni walitangaza kuupindua uongozi wake wakati akiwa kwenye matibabu nchini India.
“Leo nilishindwa kufanya mkutano na waandishi wa habari kutokana na kujisikia vibaya maana bado hali ya afya yangu tangu nitoke hospitali haijaimarika, lakini nitakapokuwa tayari nitatoa taarifa,” alisema Rage.

Comments