MASANJA MKANDAMIZAJI APANIA TAMASHA LA TUMAINI JIPYA


MCHEKESHAJI maarufu na mwimbaji wa muziki wa Injili nchini, Emmanuel Mgaya, Masanja Mkandamizaji, amesema kuwa amejipanga imara kuhakikisha kuwa anafanya vitu vya aina yake katika onyesho la Tumaini Jipya, linalotarajiwa kufanyika mkoani Morogoro Machi 31, katika Uwanja wa Jamhuri na kushirikisha pia waimbaji mbalimbali nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Masanja alisema kuwa amejiandaa vyema kutangaza neon la Mungu kwa kupitia kipaji chake cha uimbaji wa muziki wa Injili, akiamini kuwa afya yake itakuwa njema na kuimba pamoja na wadau wao katika onyesho hilo la Tumaini Jipya.
Alisema ingawa anatamba sana katika ulingo wa uchekeshaji kwa kuwa na aina ya uzungumzaji na kufurahisha watu wengi, lakini makali yake hayaelezeki katika uimbaji wa muziki wa injili.
“Nipo sawa kiafya na naamini Mungu atanibariki kila zuri kwa ajili ya kuimba pamoja kwenye tamasha hilo la Tumaini Jipya nikiwa na waimbaji wengine wenye makali ya aina yake.
“Itakuwa ni siku nzuri kwa siku ya Jumapili ya Machi 31 katika uwanja huo wa Jamhuri, hivyo naamini watu watakuja kwa wingi kulishuhudia neno likipenya masikioni mwao,” alisema Masanja Mkandamizaji.
Mbali na Masanja, wengine watakaofanya onyesho hilo ni pamoja na Martha Mwaipaja, Stara Thomas, Bahati Bukuku, Sifa John, Joseph Nyuki pamoja na vikundi mbalimbali vya kwaya vikitajwa kuwapo kwenye tamasha hilo la Tumaini Jipya litakaloanzia mkoani Morogoro.

Comments