RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar
Tenga amemshukuru Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenela
Mukangara kwa kukubali ombi la Shirikisho la kutaka kukutana naye kwa
mazungumzo na kumsihi asitishe hatua anazodhamiria kuchukua hadi hapo kikao
hicho kitakapofanyika.
Waziri Mukangara ameiagiza TFF kuitisha Mkutano Mkuu
wa marekebisho ya katiba ifikapo tarehe 15 Aprili 2013 na Mkutano Mkuu wa
Uchaguzi ifikapo tarehe 25 Mei 2013 na kwamba tamko la TFF kutekeleza maagizo
hayo liwe limetolewa katika muda wa siku tano zinazoishia Jumatatu (Machi 11,
2013).
Katika barua pepe ambayo amemuandikia Waziri ambaye kwa sasa
yuko nje ya nchi, Rais Tenga ameeleza kuwa alikwenda ofisini kwake tarehe 7
Machi 2013 kujaribu kumuona lakini akaambiwa amesafiri, hivyo kuomba kukutana
na Katibu Mkuu wa Wizara, ambaye pia hakuwepo ofisini na hatimaye akakutana na
Naibu Katibu Mkuu.
Katika barua hiyo pepe, Rais Tenga ameeleza madhumuni ya
kutaka kuonana na Waziri Mukangara kuwa ni kwanza “kukushukuru kwa kukubali
kuonana na ujumbe wa TFF ulioongozwa na mjumbe wetu wa Kamati ya Utendaji, Bw.
Alex Mgongolwa, akiongozana na Katibu Mkuu wa TFF, Bw. Angetile Osiah, jana
tarehe 6 Machi 2013.
“Kukushukuru kwa kukubali kukutana nasi tena siku ya tarehe
19 Machi, kwa ajili ya mazungumzo juu ya maagizo yako.
“Kukuarifu kuwa nimepokea maagizo yako uliyoyatoa jana
kupitia kwa Mjumbe wetu wa Kamati ya Utendaji na kwa njia ya barua; na
“Kwa heshima na taadhima, kukuomba usitishe hatua yoyote ile
unayodhamiria kuchukua hadi hapo tutakapokutana na kupata maelezo yetu, TFF,
juu ya maamuzi na maagizo uliyoyatoa.”
Tenga, ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF) aliondoka jana (Machi 7 mwaka huu) kwenda
Marrakech, Morocco kuhudhuria kikao cha kamati hiyo na pia Mkutano Mkuu wa CAF
ambao umepangwa kufanyika Machi 10 mwaka huu ukihusisha pia ajenda ya uchaguzi
wa rais.
Comments
Post a Comment