Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ametaja wachezaji 23
watakaoingia kambini Jumamosi (Machi 16 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kwa
ajili ya mechi ya mashindano dhidi ya Morocco.
Mechi hiyo ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza fainali za
Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil itachezwa Machi 24 mwaka
huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kocha Kim, wachezaji wa Taifa Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager wanatakiwa kuripoti kambini katika
hoteli ya Tansoma, Machi 17 mwaka huu.
Wachezaji walioitwa ni makipa Juma Kaseja kutoka Simba
ambaye pia ndiye nahodha wa Stars, Aishi Manula (Azam), Hussein Shariff (Mtibwa
Sugar) na Mwadini Ally (Azam). Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Erasto Nyoni
(Azam), Issa Rashid (Mtibwa Sugar), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub
(Yanga), Nassoro Masoud Cholo (Simba) na Shomari Kapombe (Simba).
Viungo ni Salum Abubakar (Azam), Athuman Idd (Yanga), Amri
Kiemba (Simba), Khamis Mcha (Azam), Frank Domayo (Yanga), Mwinyi Kazimoto
(Simba) na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar).
Washambuliaji ni John Bocco (Azam), Mbwana Samata (TP
Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mrisho Ngasa (Simba), Simon
Msuva (Yanga), na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Congo (DRC).
Mbali ya Kim, benchi la ufundi la Taifa Stars linaundwa na
Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold
Tasso (Meneja), Dk. Mwanandi Mwankemwa (Daktari wa timu), Frank Mhonda
(Mtaalamu wa tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).
SEMINA ELEKEZI COPA COCA-COLA KUFANYIKA MACHI 19
Semina elekezi kwa ajili ya michuano ya Copa Coca-Cola 2013
itafanyika Machi 19 mwaka huu jijini Dar es Salaam. Washiriki wa semina hiyo
wanatakiwa kuripoti Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) siku moja kabla
(Machi 18 mwaka huu).
Washiriki hao ni makatibu wa vyama vya mpira wa miguu vya
mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar. Pia waratibu wa mikoa wa mashindano ya Umoja
wa Michezo wa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA).
Barua za mwaliko kwa ajili ya semina hiyo tayari zimetumwa
kwa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Comments
Post a Comment