Boniface Wambura, Ofisa Habari wa TFF
SHIRIKISHO la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambalo
lilisimamisha mchakato wa uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) kutokana na baadhi ya wagombea kulalamika kuenguliwa sasa litatuma ujumbe
wake nchini katikati ya mwezi ujao.
Ujumbe huo ambao moja ya shughuli zake kuwasikiliza wote
walioenguliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF na hawakuridhika na uamuzi
huo, utakuwepo nchini Aprili 16 na 17 mwaka huu.
Kwa mujibu wa barua ya Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valcke
kwenda kwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga, kazi ya ujumbe huo ni kubaini tatizo
lililopo na kutoa ripoti kwa mamlaka zinazohusika ndani ya FIFA kwa ajili ya
kutoa mwongozo.
Ujumbe huo utakutana na pande mbalimbali zinazohusika
wakiwemo wagombea, kamati za uchaguzi za TFF. Lakini pia ujumbe huo unatarajia
kumtembelea Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella
Mukangara pamoja na watendaji wake wizarani.
Uchaguzi wa viongozi wa TFF ulikuwa ufanyike Februari 24
mwaka huu, lakini ukasimamishwa na FIFA baada ya baadhi ya wagombea
walioenguliwa kulalamika kuwa hawakutendewa haki na wangependa shirikisho hilo liingilie kati.
Comments
Post a Comment