ETOILE DU SAHEL YAITAKA SIMBA KUWA NA SUBIRA NA FEDHA ZA OKWI



KLABU ya Etoile du Sahel ya Tunisia, imewataka viongozi wa klabu ya Simba kuvuta subira kuhusu malipo ya mchezaji Emmanuel Okwi aliyejiunga na wakali hao mapema mwaka huu.
Kwa mujibu wa barua ya Machi 13, mwaka huu, iliyosainiwa na Katibu Mkuu wake Adel Ghith, kukawia kwa malipo ya nyota huyo wa kimataifa wa Uganda, ni kutokana na matizo ya taratibu
za kibenki katika kuhamisha fedha kutoka benki kuu ya nchi hiyo kuja Tanzania.
“Kwako mwenyekiti, tumekuwa tukifanya jitihada kubwa za kuhamisha fedha kutoka Benki Kuu ya hapa (Tunisia), kumekuwa na vikwazo vya kiuchumi na kisiasa, tutajitahidi kufanya kila tuwezalo kupata nyaraka muhimu Benki Kuu,” ilisema sehemu ya barua hiyo.
Adel alijinasibu kuwa kwa hadhi ya klabu yao ambayo kwa miaka 20 sasa imekuwa na wastani wa nyota watatu kila msimu, haiwezi kufanya hila kwenye jambo hilo la Okwi kwa maslahi ya pande
zote mbili.
Kiongozi huyo aliongeza kuwa changamoto za kisiasa na kiuchumi ambazo nchi ya Tunisia inapitia kwa sasa, kwa upande mwingine zinawafanya viongozi wa klabu hiyo kujituma zaidi kwa maslahi ya klabu yao na soka ya Tunisia.
Kwa barua hiyo ambayo Tanzania Daima imebahatika kuiona nakala yake, imekuja wakati ambapo suala la fedha hizo likianza kuhojiwa na wanachama wa klabu hiyo kwa hisia kuwa fedha hizo zilishatoka na zimeliwa na viongozi wa klabu hiyo.
Aidha taarifa ya Etoile du Sahel kuhusu fedha hizo, imekuja siku mbili tu tangu uongozi wa Simba utoe taarifa kuwa bado hawajalipwa fedha za Okwi na kuwasihi wadeni wake kuvuta subira kwani hivi karibuni watapata fedha zikiwemo hizo kutoka Tunisia.
Nyota huyo aliuzwa mapema mwaka huu kwa kitita cha dola 300,000 za Marekani ambazo ni sawa na shilingi mil. 450 kwa fedha za Tanzania.