EAST AFRICAN MELODY KUKINUKISHA MAX BAR KESHO

KUNDI la taarab la East african Melody 'Watoto wa Mjini' kesho
linatarajia kutimua vumbi zito la burudani, kwenye onesho lao
lililopangwa kurindima katika ukumbi wa Max Bar, Ilala bungoni, jijini
Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Melody, Hajjy Mohammed alisema jijini Dar es Salaam
jana kuwa, onesho hilo ni maalum kwa wakazi wa Wilaya Ilala pamoja na
vitongoji vyake, ajili ya kusheherekea nao Sikukuu ya Pasaka.

"Tumepokea maombi mengi ya mashabiki pamoja na wapenzi wetu wengi wa
Wilaya Ilala waliokuwa wakitaka tufurahi nao katika siku hiyo ya
Sikukuu ya Pasaka, nasi katika kuonesha kuwa tunawajali, tumeamua
kuwakubalia," alisema Hajjy.

Hajjy alisema kuwa, anaamini watamudu vilivyo kukonga nafsi za
mashabiki pamoja na wapenzi wao wote watakaohudhuria onesho hilo,
kutokana na kikosi chake kilichokusanya magwiji wengi kujipanga
vilivyo.

Alisema kuwa watakaofika kwenye onesho hilo lililopangwa kuanza
kuunguruma majira ya saa 3:30 na kuendelea hadi majogoo, watapata
fursa ya kufaidi uhondo wa vibao vyao vipya pamoja na vya zamani
vinavyoendelea kutikisa hadi sasa.