Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Beseresere imefanikiwa kutinga fainali ya
Kombe la Amani, baada ya kuichapa Fish Star kwa mikwaju ya penalti 6-5.
Awali, timu hizo zilikutana Jumapili iliyopita kwenye
Uwanja wa CCM Katoro katika mchezo wa hatua ya nusu fainali lakini mvua kubwa
iliyonyesha ikiambatana na upepo, ilisababisha mechi hiyo iahirishwe. Mpaka
pambano linakatishwa, timu hizo zilikuwa sare ya mabao 2-2.
Juzi, timu hizo zilikutana tena kwenye uwanja huo
ili kutafuta mshindi atakayetinga fainali. Mpaka dakika tisini zimalizika, zilikuwa
hazijafungana ambapo mara baada ya kuongezwa dakika 30 timu zote zilimaliza kwa
kufungana bao 1-1.
Buseresere ilipata bao lake kupitia kwa Adam
Mathias katika dakika ya 112 kwa shuti kali huku lile la Fish likifungwa na
Denis Simon katika dakika ya 114, baada ya kutokea piga nikupige katika lango
la Buseresere.
Kufuatia matokeo hayo, timu hizo ziliingia katika
changamoto ya mikwaju ya penalti ambapo Buseresere iliibuka na ushindi wa penalti
6-5.
Sasa Buseresere itaumana na Katoro katika mchezo
wa fainali Jumamosi ijayo, ikitanguliwa na mchezo wa kumsaka mshindi wa tatu
kati ya Ludete Star na Fish Star.
Mratibu wa kombe hilo linalolenga kurudisha amani
katika Kijiji cha Buseresere, Michael Izengo (Zagallo), alisema muitikio wa
watu katika michuano hiyo ni mkubwa ambapo sasa wananchi wa kijiji hicho
wamekuwa kitu kimoja tofauti na ilivyokuwa awali baada ya kutokea mauaji ya
Mchungaji Mathayo Kachila, aliyeuawa kutokana na vurugu za kidini.
Comments
Post a Comment