AZAM SWAAAAAAAAFI, SIMBA HURUMA YAO

Azam wameua 5-0, sasa wanasonga mbele Afrika

Na Waandishi Wetu
KAMA ilivyotarajiwa na wengi, Azam ndio timu pekee iliyobaki kwenye michuano ya Afrika, baada ya jioni hii kuifunga Al Nasir ya Juba, mabao 5-0 kwenye Uwanja wa Juba, Sudan Kusini.
Kwa matokeo hayo, Azam inaingia Raundi ya Pili ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa ushindi wa jumla wa mabao 8-1, kufuatia ushindi 3-1 katika mchezo wa kwanza wiki mbili zilizopita Dar es Salaam.
Azam sasa itamenyana na mshindi kati ya Al Nasir ya Libya na El Khartoum El Watan ya Sudan. Kuna uwezekano mkubwa Azam ikarejea Sudan, kwani katika mchezo wa kwanza, Al Nasir ililazimishwa sare ya bila kufungana na El Khartoum El Watan.
Katika mchezo huo, mabao ya Azam yalifungwa na Kipre Herman Tchetche, John Raphael Bocco kila mmoja mawili, moja kila kipindi na lingine Khamis Mcha ‘Vialli’.
Mapema jioni ya leo, Jamhuri ya Pemba, imekuwa timu ya kwanza ya Tanzania kuaga michuano ya Afrika, baada ya kufungwa mabao 5-0 na wenyeji Kedus Giorgis nchini Ethiopia katika mchezo wa marudiano, Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika.
Matokeo hayao, yanamaanisha, Jamhuri imeaga kwa kufungwa jumla ya mabao 8-0, baada ya awali kutandikwa 3-0 katika mchezo wa kwanza Uwanja wa Gombani, Pemba.
Wawakilishi wengine wa Bara katika michuano hiyo, Simba SC wametolewa baada ya kufungwa mabao 4-0 na Recreativo de Libolo ya Angola kwenye Uwanja wa Manispaa mjini Calulo, Angola.
Matokeo hayo, yanaifanya Simba itolewe kwa jumla ya mabao 5-0, baada ya awali kufungwa bao 1-0 Dar es Salaam.
Hadi mapumziko, Libolo walikuwa mbele kwa bao 1-0, lakini kipindi cha pili ndipo hali ikawa mbaya zaidi kwa Wekundu wa Msimbazi baada ya kutandikwa mabao hayo matatu na kuwa 4-0.
Simba ilicheza vizuri kipindi cha kwanza, lakini Recreativo walitumia zaidi upande wa kushoto kushambulia, ambako walimzidi beki Amir Maftah na kumgeuza uchochoro.
Na hata bao hilo la kwanza lilitokana na Maftah kuzembea kuokoa mpira hadi mfungaji akaingiza mguu kutokea nyuma yake na kufunga.
Kipindi cha pili, Simba ilifanya mabadiliko, ikiwatoa Amir Maftah na kumuingiza Kiggi Makassy kwenda kucheza beki ya kushoto, wakati Mrisho Ngassa alikwenda kuchukua nafasi ya Chanongo.
Mabadiliko hayo hayakuisaidia Simba SC, kwani Kiggi alikwenda kuwa uchochoro zaidi kuliko Maftah na Libolo wakapitia huko kutengeneza mabao yao, waliyoyapata dakika 15 za mwishoni.
Hata mabeki wa kati nao, waliwaruhusu wachezaji wa Angola kuruka peke yao kwenye mipira mingi ya juu, hivyo kufunga kwa urahisi. 
Kikosi cha Simba kilikuwa; Abbel Dhaira, Nassor Massoud ‘Chollo’, Amir Maftah/Kiggi Makassy, Komabil Keita, Juma Nyosso, Shomary Kapombe, Amri Kiemba, Abdallah Seseme, Haroun Chanongo/Mrisho Ngasa, Felix Sunzu na Salim Kinje.

Comments