AZAM FC:HATUJABWETEKA NA USHINDI


LICHA ya kuchanua na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya  Barrack Young Controllers II ya Liberia, wawakilishji wa Tanzania kwenye kombe la Shirikisho Barani Afrika Azam Fc, wamesema hawatabweteka na ushindi huo. 
Azam Fc ambayo ilirejea leo asubuhi kutoka Monrovia, Liberia ambapo ilikwaana na wenyeji hao jumapili iliyopita.Wanatarajiwa kurudiana hapa nchini kati ya Aprili 6 na 7 mwaka huu kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Ofisa habari wa Azam Fc Jaffer Idd, aliiambia Sports Lady kwamba, pamoja na kushukuru kwa ushindi huo alisema mchezo ulikuwa na ushindani mkubwa kwani wapinzani wao wako vizuri huku timu ikiundwa na  wachezaji wengi vijana na wenye vipaji vya hali ya juu. 
Alisema kutokana kiwango cha hali ya juu walichokiona kwa wapinzani wao hawana budi kujipanga vizuri kwa mechi ya marudiano ili kuhakikisha wanapata ushindi utakaowawezesha kusonga mbele kwenye michuano hiyo. 
“TUnashukuru tumerejea salama nchini, kikubwa tutaendelea na maandalizi yetu kama kawaida kwani tuna michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom inatusubiri tukianza na wikiendi hii na wiki ijayo kabla ya kujipanga zaidi kwa ajili ya mchezo wetu huo na Waliberia”, Alisema Idd 
Aidha, Idd amewashukuru mashabiki wa timu hiyo kwa kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa kwa wengine kwenda Liberia kuishangilia timu hiyo hivyo kuwapa ari wachezaji ya kujituma zaidi uwanjani na mwisho wa siku kuibuka na ushindi. 
Azam Fc ambayo ni timu pekee ya Tanzania inayowakilisha kwenye michuano ya kimataifa ilikutana na Waliberia hao baada ya kuondosha Al Nasr Juba Fc ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 8-1.