YANGA YAANZA KUINOLEA MAKALI AZAM FC


Kikosi cha Young Africans Sports Club
Baada ya kuichapa timu ya African Lyon kwa mabao 4-0 katika mchezo uliopita mwishoni wa wiki, Young Africans Sports Club itashuka dimbani siku ya jumamosi kucheza na timu ya Azam FC yenye makao yake chamanzi pembeni kidogo ya jiji la Dar es salam, mchezo utakaofanyika katika dimba la Uwanja wa Taifa kuanzia majira ya saa 10 jioni.
 
Young Africans ambayo inaongoza msimamo wa ligi kuu ya VPL itashuka dimbani kusaka pointi 3 muhimu ambazo zitaendelea kuifanya iendelee kuongoza msimamo wa ligi kuu lakini pia kushinda mchezo huo itakua ni kuendeleza ushindi mfululizo dhidi ya timu hiyo wa waoka mikate wa Bakhresa kwani katika michezo miwili ya mwisho, Yanga iliweza kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 kwa kila mchezo.
  
Young Africans yenye jumla ya point 36 na mabao 33 ya kufunga na mabao 12 ya kufungwa itashuka dimba la uwanja wa Taifa kuhakikisha inaibuka na ushindi katika mchezo huo dhidi ya timu ya Azam ambayo inakamata nafasi ya pilli katika msimo wa ligi kuu ya Vodacom nchini kwa kuwa na point 33.
 
Mshambuliaji Didier Kavumbagu aliyekwamisha wavuni jumla ya mabao 9 mpaka sasa, akikamata nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji mabao mengi akiwa nyuma ya mshambuliaji wa Azam Kipre Tchetche mwenye mabao 10, atakaua na fursa nzuri ya kuweza kuongeza idadi ya mabao katika mchezo huo kwani kwa hivi sasa  Didier anaonekana kuzidi kuimarika zaidi.
 
Hali kadhalika mshambuliaji aliyerudi kwa kasi katika mzunguko wa pili Jerson Tegete mwenye mabao 7 katika msimamo wa Ligi Kuu akishika nafasi ya tatu kwenye orodha ya wafungaji mabao VPL anapewa nafasi ya kuendelea kucheka na nyavu katika mchezo huo wa jumamosi.
 
Kikosi cha mholanzi Ernest Brandts kimeendelea na mazoezi leo asubuhi katika uwanja wa Mabitini Kijitonyama huku wachezaji wote wakishiriki mazoezi hayo na wakionekana kuwa wenye morali ya hali ya juu dhidi ya mchezo huo 
 
Wachezaji wote 26 wanaendelea na mazoezi ya asubuhi katika uwanja wa mabatini kijitonyama na habari njema ni kurejea uwanjani kwa mlinzi  Mbuyu Twite aliyekua majeruhi na kukosa mchezo dhidi ya African Lyon, lakini mlinzi huyo tayari amesharejea uwanjani tangu siku ya jumamosi hali inayoepelekea kikosi kizima kuwa tayari kwa maandalizi ya mchezo huo wa jumamosi.
CHANZO:www.Youngafricans.co.tz
.