YANGA WAINDEA AZAM FC BAGAMOYO


VINARA wa Ligi Kuu ya Vodacom, Yanga wameamua kwenda kambini mjini Bagamoyo kujiandaa na mechi yao dhidi ya Azam itakayochezwa Jumamosi ya wiki hii kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jana kutoka ndani ya klabu hiyo yenye maskani yake makutano ya motaa ya Twiga na Jangwani, wamekwenda huko kutokana na wachezaji kuhitaji mazingira bora na yenye utulivu.
Chanzo hicho kimedokeza kwamba, kutokana na ugumu wa mechi hiyo itakayozikutanisha timu zinazoshika nafasi mbili za kwanza katika logi hiyo, inatarajiwa kuwa yenye ushindani mkubwa.
“Unajua Azam ipo vizuri sana, imekuwa ikitoa upinzani mkubwa hasa inapokutana nasi. Tumeona ni bora wachezaji wakienda kufanya maanmdalizi tukiwa nje ya Dar es Salaa, tukiamini wachezaji watapata nafasi ya utulivu,” kilisema chanzo hicho.
Mechi hiyo inatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa kwani kila timu itahitaji kushinda ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo iliyoanza Septemba 15.
Wakati Yanga ikitaka kutwaa taji la 23 tangu kuanza kwa ligi ya taifa mwaka 1965, Azam inasaka ubingwa wa kwanza tangu kuanzishwa kwake Juni 24, mwaka 2007.
Yanga inayoongoza ligi hiyo kwa pointi 36, itakuwa ikisaka ushindi ili kuendeleza ubabe wao kwa timu hiyo kama ilivyokuwa kwenye raundi ya kwanza ya ligi hiyo ambapo Azam ilifungwa 2-0, yakifungwa na Didier Kavumbagu na Hamis Kiiza.

Comments