Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara
inamaliza raundi ya 16 kesho (Februari 13 mwaka huu) kwa mechi kati ya wenyeji
African Lyon dhidi ya Yanga itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam .
Mechi hiyo itakayochezshwa na mwamuzi Martin Saanya kutoka
Morogoro inakutanisha timu zenye mazingira tofauti. Wakati Yanga wakiwa ndiyo
vinara wa ligi hiyo kwa pointi 33, African Lyon ambayo sasa inanolewa na Salum
Bausi inakamata mkia ikiwa na pointi tisa tu.
Nayo Toto Africans itaikaribisha Polisi ya Morogoro kwenye
Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi
Jacob Adongo kutoka Musoma. Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wenye uwezo wa
kuchukua watazamaji 20,000 utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Mgambo Shooting na
Oljoro JKT.
Nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Mecky Maxime ambaye sasa
ni kocha wa Mtibwa Sugar ataiongoza timu yake hiyo katika mechi dhidi ya Ruvu
Shooting kwenye Uwanja wa Manungu ulioko Turiani, Morogoro. Ni kwenye uwanja
huo huo ambapo Mtibwa Sugar katika mechi yao
iliyopita walichapwa mabao 4-1 na Azam.
Comments
Post a Comment