UCHAGUZI TFF WASIMAMISHWA


KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF), imesitisha uchaguzi mkuu wa Shirikisho hilo uliokuwa umepangwa kufanyika Februari 24, ili kurekebisha dosari za kikanuni zilizojitokeza.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deogratius Lyato ilieleza kuwa , tarehe ya mpya ya uchaguzi huo itawekwa wazi bada ya jambo hilo kupatiwa ufumbuzi kwa nujibu wa taratubu zilizopo.
“Narudia tena, hakuna dosari kwenye kanuni, isipokuwa ni matatizo madogo madogo yaliyojitokeza wakati wa zoezi, hivyo si kwamb zoezi zima litaanza upya, hapana…litaendelea kuanzia lilipofikia sasa,” alisema Lyatto.
Alisema kamati yake imefikua uamuzi huo kwa mamlaka iliyopewa kwa mujibu wa kanuni kwani katika ibara ya 10(5), kamati yake inaruhusiwa kupangua, kubadilisha tarehe, kusimamisha au kusitisha kabisa zoezi la uchaguzi.
Lyato alisema uamuzi huo ulifikiwa na kamati yake katika kikao kilichofanyika mwishoni mwa wiki ambapo pamoja na mambo mengine, walijadili pia mchakato wa uchaguzi huo kutokana na hali iliyojitokeza.
Alisema kusitishwa kwa uchaguzi huo wa TFF kunakwenda sambamba na ule wa uchaguzi huo wa Bodi ya Ligi Kuu iliokuwa ufanyike Februari 22.
Aidha, Lyato jana alijikuta kwenye wakati mgumu pale alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa kikanuni juu ya mdau Agape Fue aliyekuwa amempinga Jamal Malinzi ambaye pingamizi lake lilitupwa na kamati yake  kwa kukosa sifa, lakini likaibukia Kamati ya Rufaa ya Idd Mtiginjola.
Akijibu swali hilo, Lyato alisema mdau huyo Agape Fue ana haki kwa kuwa alifuata kanuni ya ibara 12 (1 na 2) ya uchaguzi ambacho kinairuhusu Kamati ya Rufaa kusikiliza ombi la mtu ambaye hajaridhishwa na maamuzi ya Kamati yake.