UCHAGUZI TAFCA SASA KUFANYIKA MACHI 16


Eugine Mwasamaki, Katibu Mkuu wa TAFCA
Baada ya kukwama mara mbili, wanachama wa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu (TAFCA) wamepewa fursa ya kufanya uchaguzi wa chama hicho Machi 16 mwaka huu mjini Dodoma.

Kwa mujibu wa tangazo la uchaguzi huo, fomu kwa ajili ya waombaji uongozi katika TAFCA zitaaza kutolewa kesho (Febaruari 7 mwaka huu) na mwisho wa kurudisha ni Februari 11 mwaka huu. Majina ya waombaji uongozi watakaokuwa wamepitishwa yatatangazwa Februari 12 mwaka huu.

Kipindi cha kuweka pingamizi ni kuanzia Februari 13 hadi 17 mwaka huu. Usaili kwa waombaji utafanyika Februari 19 mwaka huu wakati matokeo ya usaili yatatangazwa Februari 20 mwaka huu.

Kamati ya Uchaguzi ya TFF itasikiliza rufani kama zitakuwepo kati ya Februari 20 na 22 mwaka huu, na uamuzi wa rufani hizo utatangazwa kati ya Februari 23 na 27 mwaka huu.

Ada za fomu kwa waombaji uongozi zitakuwa sh. 200,000 kwa nafasi zote isipokuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF na wajumbe wa Kamati ya Utendaji. Nafasi zitakazowaniwa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mhazini, Mhazini Msaidizi, Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF na wajumbe wa Kamati ya Utendaji.

Fomu kwa waombaji uongozi zinapatikana kwenye ofisi za TAFCA zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.

Comments