TFF YAZITAKIA HERI SIMBA, AZAM FC KIMATAIFA, YASISITIZA WATANZANIA KUWA WAZALENDO


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limezitaka timu za Azam Fc na Simba kuutumia vema uenyeji wake kwa kuhakikisha zinashinda mechi zake za kimataifa zitakazopiugwa mwishoni mwa wiki hii.
Wakati Azam Fc itashuka jumamosi kwenye uwanja wa Taifa kuikabili Al Nasri Juba Sudani Kusini katika kombe la Shirikisho, Simba itashuka jumapili kwenye uwanja huo kuivaa Recretivo de Libolo ya Angola katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah amesema leo kwamba anaamini Azam na Simba zimejipanga vema kwa mechi hizo ambazo zitakuwa na uopinzani mkubwa kwani timu wanazokutana nazo zinatoka ukanda wenye upinzani.
“Juba inashiriki kwa mara ya kwanza michuano ya kimataifa baada ya nchi yao kupata uanachama wa FIFA mwaka jana na nnaamini watakuwa wamejipanga, hata hawa wapinzani wa Simba si timu ya kubeza pia hivyo Simba nayo ina mtihani mkubwa,”alisema
Aidha, Osiah aliwataka mashabiki wa soka nchini kuacha siasa za Usimba na Uyanga kwa kuzomea uwanjani wakati timu hizo zitakapoishuka badala yake kuungana pamoja kuzishangilia ili kuwapa nguvu wachezaji.
“Hizi timu ni za Tanzania kama zitashinda sifa itakuja kwa Tanzania na kama zitashindwa aibu itakuja kwa Tanzania na si timu, hivyo nawaomba mashabiki tuache tabia za kuzomea hovyo uwanjani,’alisema
Aidha, Osiah amewaomba viongozi wa timu za Azam na Simba kutotengeneza mazingira ya kihasama kwa timu opinzani badala yake kuzipa ushirikiano wa kutosha tangu zinapotua nchini hadi kuondoka kwake baada ya mechi.