Rais wa TFF Leodger Tenga kulia akizungumza na waandishi wa habari leo, kushoto ni Katibu wa TFF, Angetile Osiah
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo mchana, Rais Tenga amesema TFF ni moja ya taasisi ambazo zina utaratibu
unaoeleweka kwa wadau wake.
“Wote tunafahamu taratibu ambazo tumejiwekea juu ya wagombea
wetu wanachaguliwaje. TFF ni moja ya taasisi ambazo zina utaratibu unaoeleweka.
Hii ni kuanzia wilayani. Kama kuna tatizo zipo
njia za kufuata.
“Katika mchakato wa uchaguzi wengine wanafanikiwa, wengine
wanaachwa. Wameachwa kwa sababu zilizotolewa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi.
Ambaye haridhiki anafuata taratibu tulizojiwekea. Atafute haki yake kwa mujibu
wa taratibu,” amesema.
Rais Tenga amesisitiza kuwa kikatiba hana uwezo wa kuingilia
uamuzi unaofanywa na kamati ambazo ameziunda, kwani utawala bora ni kusimamia
kanuni ambapo wanaofanya uamuzi lazima waweke wazi sababu za uamuzi waliofikia.
Amesema ambao hawakubaliani na uamuzi wa Kamati ya Rufani ya
Uchaguzi ya TFF dhidi yao
wana njia tatu za kufuata. Njia hizo ni kuiomba Kamati ya Rufani ya Uchaguzi
ipitie uamuzi iliofanya (review), kuandika Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa
Miguu (FIFA) kuomba liingilie au kwenda Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo
(CAS).
“Hata ukiweka ngazi nne, mtu akiathirika ataona ameonewa tu.
Kwa Katiba yetu hapa (Kamati ya Rufani ya Uchaguzi) ndiyo mwisho. Hakuna chombo
kingine. Ukiwaomba FIFA waingilie, watakuja na tutawaeleza mchakato wote
ulivyokwenda. Tunapenda kuwahakikishia hawa (waathirika) kuwa kwa maslahi ya
mpira wa miguu tutasaidia katika hilo
wapate haki,” amesema Rais Tenga na kuongeza kuwa tayari waathirika wawili wa
uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi wameomba marejeo (review) kwenye kamati
hiyo hiyo.
Amesema TFF imelazimika kuzungumzia suala hilo kwa sababu limekuwa likizungumzwa kinazi
zaidi wakati taratibu ziko wazi, hivyo kwa maslahi ya mpira wa miguu ni vizuri
taratibu zikafuatwa.
“Nawaomba washabiki wa mpira wa miguu, tumejenga chombo hiki
(TFF) kwa muda mrefu. Bado tunaomba watu watusaidie, kwa hiyo matusi hayawezi
kubadili kitu. Tunachowahakikishia ni kuwa, mtu anapoomba msaada tutampa
kutafuta haki yake.
“Hizi ni kamati huru, lazima ziheshimiwe. Ukianza
kuziingilia utakuwa umeua mpira wa miguu. Uongozi ni utumishi, tusionekane
tunagombana. Huu si ubunge, mbunge anachaguliwa anakwenda kulipwa mshahara.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF halipwi mshahara. Tusirudi kwenye matusi,
tulishaondoka huko,” amesema.
Kuhusu mabadiliko ya Katiba yaliyofanyika kwa njia ya
waraka, Rais Tenga amesema yamefanyika kwa mujibu wa taratibu, na haikuwa siri.
Maeneo yaliyofanyiwa marekebisho ilikuwa ni lazima, kwani mengi yalikuwa ni
maagizo kutoka FIFA na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Amesisitiza kuwa mabadiliko hayo yamefuata taratibu na
hakuna udanganyifu katika hilo ,
kwani ridhaa ya kutumia waraka iliombwa, na Mkutano ni watu ambao ndiyo
wamepitisha mabadiliko hayo.
“Mkutano Mkuu ni watu, si kikao. Katika dunia ya leo
mikutano inafanyika kwa tele conference, si lazima watu wakutane sehemu moja,”
amesema na kuongeza kuwa mabadiliko hayo yalipitishwa kwa kura 70 dhidi ya 33
zilizokataa.
Kuhusu Kanuni kusainiwa kabla ya Katiba, Rais Tenga amesema
tarehe ya kuanza kutumika Katiba ni siku ridhaa ilipopatikana, na si siku mhuri
wa Msajili ulipopigwa. Mabadiliko ya Katiba yalipita Desemba 15 mwaka jana,
Kanuni zilisainiwa Januari 7 mwaka huu.
Comments
Post a Comment