SIMBA SARE 1-1 NA OLJORO

Amri Kiemba, akimpongeza Mwinyi Kazimoto baada ya kufunga. Kushoto ni beki wa Oljoro Salim Mbonde na kulia ni Mussa Mudde na Rashid Ismail (6).   

Na Mahmoud Zubeiry, Arusha
SIMBA SC imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na JKT Oljoro ya Arusha, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini hapa jioni hii.
Hiyo inakuwa sare ya pili mfululizo wa mabingwa hao watetezi, baada ya wiki iliyopita kulazimishwa sare kama hiyo na JKT Ruvu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matokeo hayo, yanaifanya Simba itimize pointi 28, baada ya kucheza mechi 16, hivyo kuzidi kuliweka rehani taji lake la ubingwa, kwani wapinzani wao wa jadi, Yanga wanaongoza kwa pointi 33 na mchezo mmoja mkononi, wakati Azam FC ya pili kwa pointi 30 na mchezo mmoja mkononi pia.
Simba iliuanza vizuri mchezo wa leo, ikishambulia mfululizo langoni mwa Oljoro na ikafanikiwa kupata bao la mapema tu dakika ya saba, lililofungwa na kiungo Mwinyi Kazimoto.
Kazimoto alifunga bao hilo kwa shuti la umbali wa mita 20 na ushei, baada ya kumchungulia kipa wa Oljoro, Said Lubawa na kuupeleka mpira juu kushoto.
Lilikuwa shuti kali ambalo lilipenya kwenye nyavu zilizozeeka za Uwanja wa Sheikh Amri Abeid na kuwachanganya mashabiki wakidhani mpira umetoka nje.
Hadi mapumziko, Simba walikuwa mbele kwa bao hilo 1-0 na kipindi cha pili ndipo Oljoro waliporekebisha makosa yao na kufanikiwa nao kupata bao la kusawazisha.
Alikuwa Paul Nonga katika dakika ya tisa tu tangu kuanza kipindi cha pili aliyezima ndoto za Wekundu wa Msimbazi kuondoka na pointi tatu kwenye mchezo wa leo, baada ya kuifungia bao Oljoro.
Katika mchezo huo, Oljoro waliipunguza kasi Simba kwa kupiga viatu, ambavyo vilimfanya beki Paul Ngalema aliyekuwa akipanda mno kusaidia mashambulizi asimalize dakika 45 za kipindi cha kwanza baada ya kuumizwa dakika ya 23.
Kitu kingine kilichoonekana dhahiri kuiathiri Simba katika mchezo wa leo, pamoja na uchezeshaji mbovu wa marefa, lakini ni aina ya uchezaji wao wa mipira ya pasi za chini na Uwanja mbovu wa Sheikh Amri Abeid.
Katika dakika ya 68, beki Shaibu Nayopa aliunawa mpira kwenye eneo la hatari, tena ndani ya sita, lakini refa Athumani Lazi akapeta, licha ya wachezaji wa Oljoro kuonekana kuzubaa kwa sekunde kadhaa wakiamini ni penalti. 
Katika mchezo wa leo, kikosi cha Simba SC kilikuwa; Juma Kaseja, Nassor Masoud 'Chollo', Paul Ngalema/Emily Mghtto, Komabil Keita, Shomary Kapombe, Mussa Mudde/Abdallah Seseme, Haroun Chanongo, Rashid Ismail/Mrisho Ngassa, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto na Amri Kiemba.
JKT Oljoro; Said Lubawa, Yussuf Machugu, Majaliwa Mbaga, Nurdin Suleiman, Shaibu Nayopa, Salim Mbonde, Kalaghe Gunda/Marcus Raphael, Emanuel Memba/Hamisi Saleh, Paul Nonga na Sanu Mwaseba.

Comments