SIMBA HAOOO UINGEREZA, USO KWA USO NA SUNDERLAND


UONGOZI wa klabu ya Simba unatarajiwa kwenda nchini Uingereza kwa ajili ya kukutana na uongozi wa timu ya Sunderland  inayoshiriki ligi kuu ya huko.
Aidha, Simba imemshukuru Rais wa Tanzania Jakata Mrisho Kikwete  ambaye alimkutanisha mwenyekiti wa Simba, Aden Rage na mwenyekiti wa Sunderland, Ellis Short ambaye alikuja nchini.
Ofisa habari wa Simba Ezekiel Kamwaga amesema leo kwamba hatua ya uongozi wa Simba kwenda huko inafuatia hatua nzuri ya mazungumzo ya ushirikiano baina ya pande hizo mbili.
“Kwa kweli tunamshukuru sana Rais Kikwete kwa kumkutanisha mwenyekiti wetu Rage na Short na ndipo mambo haya mazuri yakajitokeza,”alisema
Alisema ni matarajio yao klabu ya Simba itapiga hatua kubwa kupitia ushirikiano na timu hiyo kongwe nchini Uingereza kwani tayari wameshaanza kukubaliana baadhi ya mambo ikiwemo uendelezaji wa soka la vijana.
Kamwaga aliongeza kuwa uongozi wa Simba utakapokuwa nchini Uingereza pamoja na kushuhudia baadhi ya mechi za timu hiyo, pia utapata fursa ya kubadilishana uzoefu wa kiuongozi  na wenyeji wao.

Comments