SIMBA CHALI KWA LIBOLO

Libolo wakishangilia ushindi wao Uwanja wa Taifa leo

Na Mahmoud Zubeiry
BAO pekee la Joao Martins dakika ya 24, leo limeizamisha Simba SC katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza, Ligi ya Mabingwa Afrika mbele ya Recreativo de Libolo ya Angola, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hadi mapumziko, Recreativo de Libolo walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na mshambuliaji huyo hodari, aliyeunganisha kwa kichwa krosi ya Dario Cardoso kutoka wingi kulia.
Kapombe akiugulia maumivu baada ya mechi kwa kilio
Kwa ujumla, Libolo waliizidi Simba dakika 45 za kwanza, na zaidi kukosekana kwa mashambulizi ya kusisimua, kulitokana na Simba kukosa nguvu katika safu ya ushambuliaji.
Mrisho Ngassa na Haruna Chanongo waliokuwa wakishambulia kutokea pembeni, walijitahidi kutia krosi kwenye lango la Libolo, lakini mshambuliaji pekee Haruna Moshi ‘Boban’ alidhibitiwa vikali na mabeki wa Libolo.
Kipindi cha pili, Simba walirekebisha makosa yao na kuanza kufanya mashambulizi ya maana langoni mwa Libolo, lakini umaliziaji mbovu na uimara wa kipa Landu Mavanga uliwakosesha mabao.
Baada ya kosa kosa nyingi langoni mwa Libolo, dakika tano za mwisho Simba walionekana kukata tamaa na kuwaacha wapinzani kutawala mchezo.
Matokeo haya, yanamaanisha Simba sasa inahitaji kushinda mabao zaidi ya 2-0 katika mchezo wa marudiano wiki mbili zijazo Angola ili kusonga mbele. 
Baada ya mchezo huo, beki wa Simba, Shomary Kapombe alianguka na kuanza kulia akilalamikwa kubanwa misuli.
Daktari wa Simba SC, Cossmas Kapinga alimuwahi kumpatia huduma ya kwanza hadi hali yake ikawa njema.  
Katika mchezo wa leo, kikosi cha Simba SC kilikuwa; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Shomary Kapombe, Komabil Keita, Juma Nyosso, Mussa Mudde/Amir Maftah dk53, Mrisho Ngassa, Amri Kiemba, Haroun Chanongo/Ramadhan Singano ‘Messi’ dk66, Mwinyi Kazimoto na Haruna Moshi ‘Boban’/Salim Kinje dk 84.
Libolo; Landu Mavanga, Carlos Almeida, Anotnio Cassule, Pedro Libeiro, Gamaliel Massumari, Manuel Lopez, Sidnei Mariao, Dorivaldo Dias, Joao Martins/Andres Madrid dk72, Dario Cardoso/Muno Silva dk82 na Maieco Antonio/Henry Camara dk76