SIMBA 1-1 JKT RUVU

Kiungo wa Simba, Amri Kiemba akiwapiga chenga beki Jimmy Shoji na kipa Shaaban Dihile, kabla ya kuifungia bao la kuongoza Simba SC.


Na Mahmoud Zubeiry
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba SC leo wamelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na JKT Ruvu ya Pwani katika mchezo wa Ligi Kuu uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matokeo haya yanaiongezea pointi moja tu Simba SC na sasa imetimiza 27, baada ya kucheza mechi 15, ikiendelea kushika nafasi ya tatu, nyuma ya Azam yenye 30 na Yanga 32.
Hadi mapumziko, Simba walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na kiungo Amri Ramadhan Kiemba, aliyewapiga chenga beki Jimmy Shoji na kipa Shaaban Dihile dakika ya 17, kabla ya kutumbukiza mpira nyavuni.
Kwa ujumla Simba walicheza vema kipindi cha kwanza, wakitawala safu ya kiungo na gonga zao safi za uhakika na kama wangekuwa makini wangeweza kutoka uwanjani baada ya nusu hiyo ya kwanza wakiwa na hazina kubwa ya mabao.
Kipindi cha pili mchezo ulibadilika na zaidi Simba ilionekana kuathiriwa na mabadiliko ya wachezaji iliyomfanya, haswa kumtoa Mrisho Ngassa aliyekuwa akiisumbua ngome ya JKT.
Maafande hao wa Ruvu walizidisha kasi ya mashambulizi langoni mwa Simba, wakiamini Wekundu wa Msimbazi hawana mtu hatari mbele.
Hilo liliisaidia timu hiyo kupata bao la kusawazisha dakika ya 63, lililofungwa na Nashon Naftali akiunganisha krosi ya Mussa Hassan Mgosi.
Baada ya kufungwa bao hilo, Simba walicharuka kusaka bao la ushindi, lakini jitihada zao ziliishia kwenye ngome ya JKT iliyokuwa imara kipindi cha pili na kutorudia makosa ya kipindi cha kwanza.
Refa Alex Mahagi wa Mwanza aliwapa Simba penalti dakika ya 87, baada ya beki Damas Makwaya kugongana na Haruna Moshi ‘Boban’ kwenye eneo la hatari.
Nahodha Msaidizi wa Simba SC, Shomary Kapombe alikwenda kupiga penalti yake vizuri, lakini kipa Shaaban Dihile aliipangua ikagonga mwamba na kurudi uwanjani, akaichupia kuidaka.
Simba SC hawakukata tamaa hata baada ya kukosa penalti dakika za lala salama, waliendelea kufanya mashambulizi ya haraka haraka kusaka  bao, lakini bahati haikuwa yao.   
Katika mchezo huo, kikosi cha Simba SC kilikuwa; Juma Kaseja, Haruna Shamte, Paul Ngalema, Shomary Kapombe, Komabil Keita, Abdallah Seseme/Haruna Moshi, Haroun Chanongo, Mwinyi Kazimoto, Mrisho Ngassa/Abdallah Juma, Amri Kiemba, Ramadhan Chombo/Kiggi Makassy.
JKT Ruvu; Shaaban Dihile, Credo Mwaipopo, Kessy Mapande, Kisimba Luambano, Damas Makwaya, Jimmy Shoji, Hussein Bunu, Nashon Naftali, Mussa Mgosi, Zahor Pazi na Emmanuel Pius.

Comments