Washambuliaji wa Taifa Stars, Mbwana Samata na Thomas
Ulimwengu wanatarajia kutua nchini kesho (Februari 3 mwaka huu) tayari kwa
mechi ya Cameroon itakayochezwa Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Samata na Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) watawasili saa 11.10 jioni kwa ndege ya
PrecisionAir na kwenda moja kwa moja kambi hoteli ya Tansoma.
Wachezaji wa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium
Lager wanaanza kuripoti kambini leo jioni (Februari 2 mwaka huu) mara baada ya
mechi kati ya Yanga na Mtibwa Sugar.
Mechi hiyo iliyo katika Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa
la Mpira wa Miguu (FIFA) pia itatumika kwa ajili ya kutoa ujumbe wa vita dhidi
ya Malaria viwanjani, ugonjwa unaoongoza barani Afrika kwa kusababisha vifo vya
watoto na wajawazito.
TFF kama ilivyo Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika
Mashariki na Kati (CECAFA), Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na FIFA
imekuwa msitari wa mbele katika kueneza kampeni ya vita dhidi ya Malaria
inayoongozwa United Against Malaria (UAM). Rais wa TFF, Leodegar Tenga na
nahodha wa Cameroon, Samuel Eto’o ni miongoni mwa mabalozi wa vita dhidi ya
Malaria barani Afrika.
Comments
Post a Comment