MUSA KISSOKY MWENYEKITI MPYA SPUTANZA


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Wachezaji Mpira wa Miguu Tanzania (SPUTANZA) na wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) uliochaguliwa wiki iliyopita. 
Uongozi wa FRAT ulichaguliwa Februari 13 mwaka huu mjini Morogoro wakati wa SPUTANZA ulichaguliwa jana (Februari 17 mwaka huu) katika uchaguzi uliofanyika Kigamboni, Dar es Salaam. 
Waliochaguliwa kuongoza SPUTANZA na hawakuwa na wapinzani ni Musa Kissoky (Mwenyekiti) na Said George (Katibu Mkuu) wakati Ali Mayai aliwashinda Isaac Mwakatika na Hakim Byemba katika nafasi ya mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF. 
Kusianga Kiata na Charles Mngodo walichaguliwa kuwa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya SPUTANZA. Katika uchaguzi huo uliohudhuriwa na wapiga kura 17, Mhazini na nafasi moja ya mjumbe wa Kamati ya Utendaji zitajazwa baadaye kutokana na kukosa wagombea. 
Kwa upande wa FRAT viongozi waliochaguliwa ni Said Nassoro (Mwenyekiti), Charles Ndagala (Katibu Mkuu) na Kamwanga Tambwe (mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF). 
Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza vyama hivyo unaonesha jinsi wapiga kura walivyo na imani kubwa kwao, na TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya FRAT na SPUTANZA. 
Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu kwa kuzingatia katiba zao pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yao. 
Pia tunatoa pongezi kwa kamati za uchaguzi za FRAT na SPUTANZA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi umeendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.