MARUFUKU WAGOMBEA KUFANYA KAMPENI-TFF


SHIRIKISHO la soka Tanzania (TFF) limepiga marufuku kwa wagombea uongozi wa Shirikisho hilo kufanya kampeni kwa sasa na atakayebainika kufanya hivyo kamati ya uchaguzi itamuondoa kwenye kinyang’anyiro hicho. 
 Ofisa habari wa TFF, Boniface Wambura alisema kwamba kampeni bado zimesimamishwa hivyo hairuhusiwi mtu yoyote kufanya kampeni mpaka itakapoangazwa. 
“TUnapenda kuwakumbusha wale waliopitishwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi TFF kutoendesha kampeni kwa sasa mpaka watakapopewa barua za ruhusa hiyo na yeyote atakayekiuka kamati ya uchaguzi inamamlaka ya kumuengua katika kinyang;’anyiro hicho. 
Hivi karibuni, kamati ya uchafguzi ya TFF chini ya mwenyekiti wake Deo Lyatto ilitangaza kusitisha kampeni za wagombea wa uchaguzi wa viongozi wa TFF uliopangwa kufanyika Februari 24 pamoja na ule wa bodi ya ligi uliopangwa kufanyika Februari 22. 
Aidha, kumekuwa na sintofahamu juu ya uchaguzi huo baada ya hivi karibuni kuwepo kwa shinikizo la kutaka kurejeshwa kwa aliyekuwa mgombea nafasi ya Urais wa TFF,Jamal Malinzi ambaye jina lake lilienguliwa na kamati ya Rufaa. 
Kitendo cha kuenguliwa kwa Malinzi kimeibua hisia tofauti kwa wadauy wa soka ambao kwa nyakati tofauti wameinyooshea kidole TFF juu ya suala hilo kwa madai kwamba imeingiza mkono katika hilo, huku wakipanga kwenda kuzuia uchaguzi huo magakamani iwapo hatarejeshwa kwenye kinyang’anyiro hicho. 
Kama hiyo haitoshi, mmoja ya wagombea aliyeenguliwa katika kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Michael Wambura naye ameitaka TFF kuifuta kamati ya Rufaa kwa madai kuwa si halali, huku akipendekeza uchaguzi huo kufanywa kwa kufuata kanuni za zamani.