Kocha Mkuu wa Azam, Stewart John Hall amefungiwa mechi tatu
na kupigwa faini ya sh. 500,000 kwa kushusha bukta yake na kumlalamikia mwamuzi
msaidizi wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya timu yake na
Kagera Sugar iliyochezwa Januari 26 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex ulioko
Chamazi, Dar es Salaam .
Adhabu hiyo imetolewa na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana mwishoni mwa wiki kupitia ripoti za
michuano ya VPL na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2012/2013 inayoendelea
hivi sasa na kufanya uamuzi mbalimbali.
Naye Kocha Msaidizi wa timu ya Mgambo Shooting, Denis
Mwingira ametozwa faini ya sh. 500,000 kwa kumtolea lugha chafu mwamuzi kwenye
mechi dhidi ya Mtibwa Sugar iliyochezwa Oktoba mwaka jana katika Uwanja wa
Manungu.
Ally Jangalu ambaye ni Kocha Msaidizi wa Polisi Morogoro
naye ameangukiwa na rungu la Kamati ya Ligi kwa kupigwa faini ya sh. 500,000
baada ya kutolewa kwenye benchi kwa kupinga uamuzi wa refa kwa sauti ya juu.
Alitenda kosa hilo kwenye mechi kati yao na Kagera Sugar
iliyochezwa Novemba 10 mwaka jana Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Matukio ya aina hiyo kwa kocha Jangalu yamekuwa ya
kujirudiarudia ambapo Oktoba 13 mwaka jana katika mechi dhidi ya Azam
iliyochezwa mjini Morogoro aliondolewa na mwamuzi kwenye benchi kwa kuchochea
wachezaji wa timu yake wacheze rafu.
Naye Kocha wa timu ya Moro United inayoshiriki FDL, Yusuf
Macho amepigwa faini ya sh. 200,000 kwa kumtolea lugha chafu refa baada ya
mechi dhidi ya Transit Camp
iliyofanyika Novemba 4
mwaka jana Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi.
Pia Kocha wa Burkina
Faso , Hasheem Mkingie amepigwa faini ya sh.
200,000 baada ya kutolewa kwenye benchi kwa kutoa lugha chafu katika mechi ya
FDL dhidi ya Mkamba Rangers.
Kiongozi wa Majimaji, Joseph Nswila ambaye aliingia uwanjani
baada ya mechi dhidi ya Mlale JKT kumalizika na kuvamia waamuzi amefungiwa
miezi sita.
Vilevile timu ya Azam imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa
kuchelewa kufika uwanjani kwenye mechi kati yao
na JKT Oljoro iliyochezwa Novemba 7 mwaka jana katika Uwanja wao wa Azam
Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam .
Pia Coastal Union imetozwa faini ya sh. 500,000 kutokana na
washabiki wake kumrushia chupa za maji mwamuzi msaidizi namba mbili wakati wa
mechi yao dhidi
ya Simba iliyochezwa Oktoba mwaka jana Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Nayo klabu ya African Lyon imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa
timu yake kugoma kuingia kwenye chumba cha kubadilishia nguo wakati wa
mapumziko katika mechi dhidi ya Coastal Union iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani
jijini Tanga, Oktoba 24 mwaka jana.
Timu ya Burkina Faso
ya Morogoro imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na kuonesha vitendo vya
ushirikina kabla ya mechi yao dhidi ya Mbeya City
iliyochezwa Oktoba 24 mwaka jana Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Faini ya ushirikina ya sh. 200,000 pia imepigwa timu ya
Pamba baada ya kuonesha vitendo hivyo kwenye mechi yao dhidi ya Mwadui iliyochezwa Novemba 4
mwaka jana Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Nayo Mkamba Rangers imepigwa faini ya sh. 200,000 baada ya
washabiki wake kumtolea lugha chafu Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa
Morogoro (MRFA), Hamis Semka na kumrushia chupa za maji mwamuzi wa mezani
katika mechi dhidi ya Mbeya
City iliyochezwa mjini
Morogoro.
Polisi Dodoma imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na
washabiki wake kuvamia uwanjani na kutaka kuwapiga waamuzi katika mechi yao dhidi ya JKT Kanembwa na kusababisha mipira miwili ya
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dodoma
(DOREFA) kupotea.
Pia klabu kadhaa zimeandikiwa barua za onyo kwa timu zao
kuchelewa kufika uwanjani au kutofika kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi
(Pre-match meeting). Klabu hizo ni Coastal Union, JKT Ruvu, Toto Africans,
Simba, Green Warriors, Majimaji, Mkamba Rangers, Polisi Dodoma, JKT Kanembwa,
Moro United.
Mchezaji Stanley Nkomola wa JKT Ruvu baada ya mechi dhidi ya
Coastal Union alikwenda jukwaani na kuanza kupigana na washabiki. Pia kipa wa
timu ya Transit Camp, Baltazar Makene baada ya mechi dhidi ya Tessema aliruka
uzio na kwenda kupigana na washabiki.
Kwa vile masuala ya wachezaji hao ni ya kinidhamu
yamepelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu inayoongozwa na Kamishna wa Polisi (CP)
mstaafu Alfred Tibaigana kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.
Comments
Post a Comment