KMKM YAANZA VEMA LIGI KUU ZENJI KWA KUICHAPA MAFUNZO


Na Ally Mohammed, Zanzibar
MZUNGUKO wa Pili wa Ligi Kuu ya Zanzibar maarufu Zanzibar Grand Malt
Premier League, umeanza rasmi hapo jana kwa michezo miwili katika viwanja viwili tofauti ndani ya visiwa vya Unguja na Pemba.

Tukianzia katika uwanja wa Mao Tse Tung, Kisiwani Unguja, vinara wa ligi hiyo KMKM waliteremka uwanjani hapo kucheza na Mafunzo, pambano ililomalizika kwa KMKM kuibuka kidedea baada ya kuifunga Mafunzo mabao 2-1.
KMKM ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wao tegemeo Maulid Ibrahim katika dakika ya 35 ya kipindi cha kwanza, mpaka mapumziko matokeo yalikuwa yanasomeka 1-0.
Kipindi cha pili katika mchezo huo kiliingia dosari baada ya mchezaji wa KMKM Faki Mwalim kutolewa nje kwa kadi nyekundu kufuatia mchezo mbaya.
Mafunzo walifanikiwa kusawazisha katika dakika ya 79 kupitia kwa Ame Khamis, hata hivyo bao hilo halikudumu kwani licha ya KMKM kucheza pungufu kwa mchezaji mmoja walifanikiwa kupata bao la ushindi katika dakika ya 82 kupitia kwa Jaku Joma.
Kwa matokeo hayo KMKM wanaendelea kuongoza msimamo wa ligi hiyo baada ya kufikisha pointi 26 wakifuatiwa na Mafunzo yenye pointi 22.

Huko kisiwani Pemba katika uwanja wa Gombani, mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Super Falcon wamefanikiwa kuanza vyema mzunguko wa pili baada ya leo kuchomoza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Chipukizi ya Chake Chake.

Bao pekee la ushindi kwa Super Falcon lilifungwa katika dakika na Omar Mohammed katika dakika ya 69.
Ligi hiyo inatarajia kuendelea tena leo katika viwanja viwili.
--