KAPOMBE, MESSI KUJARIBIWA SUNDERLAND

 Mwenyekiti wa simba, Ismail Aden Rage pamoja na mfadhili wa timu hiyo, Rahma Alkharoos wakinesha moja ya jezi watakazopewa na tim,u ya Sunderland ya Uingereza kama sehemu ya ufadhili wao.

 WACHEZAJI chipukizi wa timu ya soka ya Simba Ramadhan Singano ‘Messi’ na Shomari Kapombe wanatarajiwa kwenda kufanya majaribio katika kituo maalum cha vijana cha klabu inayoshiriki Ligi Kuu ya England, Sunderland. 
Aidha, viongozi wa Simba, wanatarajiwa kwenda huko hivi karibuni  ambapo pamoja na mambo mengine watashuhudia mechi ya ligi kuu ya England baina ya wenyeji Sunderland dhidi ya Fulham itakayopigwa Machi 2 mwaka huu. 
Mwenyekiti wa Simba Alhaj Ismail Aden Rage alisema, hatua hiyo inafuatia ushirikiano baina yao na Sunderland uliotokana na matunda ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete. 
Alisema katika makubaliano yao ya ushirikiano na udhamini, Sunderland ambayo imepania zaidi kuwekeza katika soka la vijana ambapo itakuwa ikichukua wachezaji katika makundi tofauti ya umri wa klabu ya Simba na kwenda kujifunza katika taasisi yao ya vijana. 
Rage aliongeza kuwa, Kapombe na Singano watakwenda huko mara baada ya kumalizika kwa ligi kuu ya Vodacom ambapo pamoja na kupatiwa mafunzo maalum katika kituo cha kulea vijana cha timu hiyo, kama watafanya vema katika mazoezi yao huenda wakasajiliwa kuichezea timu ya vijana ya Sunderland. 
Aidha, Rage aliongeza kuwa mazungumzo kuhusiana na udhamini wao na Sunderland yapo katika hali na ndiyo maana uongozi umealikwa kwenda huko si kwa ajili tu ya kushuhudia mechi bali kubadiklishana uzoefu na viongozi wa timu hiyo.