YONDAN, DOMAYO WAONGEZA MAKALI STARS, TIMU KWENDA ETHIOPIA KESHO


WAKATI kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kikitarajiwa kuondoka alasiri ya kesho kwenda Ethiopia, Yanga imeruhusu nyota wake wawili kati ya watano walioitwa kwenye kikosi hicho.
 Yanga ambayo imepiga kambi ya maandalizi nchini Uturuki ilizuia nyota wake kujiunga na kambi ya Stars iliyoanza jumapili iliyopita jijini Dar es Salaam kujiandaa na mchezo huo utakaopigwa keshokutwa katika uwanja wa Taifa wa Addis Ababa.
Ofisa habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Boniface Wambura ameiambia Sports Lady kwamba baada ya mazungumzo baina ya kocha mkuu wa Stars Kim Poulsen na yule wa Yanga Ernie Brandts, walikubaliana beki Kelvin Yondan na Kiungo Frank Domayo wa Yanga ndio wajiunge na Stars. 
Yondan na Domayo wanatarajiwa  kuwasili nchini usiku wa leo na endapo watachelewa watakwenda Ethiopia peke yao.Wachezaji wengine wa Yanga walioitwa Stars ambao wataendelea kubaki nchini Uturuki ni pamoja na Athuman Iddy ‘Chuji’, Simon Msuva na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ watakaojiunga na Stars watakaporejea nchini Januari 13 kutoka Uturuki. 
Mchezo huo ni maalum kwa kuipa maandalizi ya mwisho Ethiopia kabla ya kwenda Afrika Kusini kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazoanza Januari 19 mwaka huu.
 Aidha, Wambura aliongeza kuwa, tayari wachezaji wa Simba,  Azam Fc na Mtibwa Sugar waliokuwa Zanzibar na timu zao zinazoshiriki michuano ya kombe la Mapinduzi inayoendelea Visiwani Zanzibar waliwasili mchana wa leo  na kuungana na wenzao. 
“Hata hivyo Azam  Fc imeruhusu kipa mmoja tu Aishi Manula huku Mwadini Ally ambaye pia aliitwa Stars ataendelea kubaki na timu kwenye kombe la Mapinduzi,”alisema Wambura 
Aliwataja wengine wachezaji waliopo ni pamoja na Juma Kaseja kutoka Simba ambaye pia ndiye nahodha wa Stars na  Manula ( Azam FC), huku kwa upande wa Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Amir Maftah (Simba), Erasto Nyoni (Azam), Issa Rashid (Mtibwa Sugar), na Shomari Kapombe (Simba). 
Viungo ni Salum Abubakar (Azam), Amri Kiemba (Simba), Khamis Mcha (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba) na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), wakati washambuliaji ni Mbwana Samata, Thomas Ulimwengu  (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC) na  Mrisho Ngasa (Simba). 
Stars ambayo pia itautumia mchezo huo kama sehemu ya maandalizi ya mechi ya mchujo dhidi ya Morocco kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia 2014, mchezo utakaochezwa Machi mwaka huu. 
Katika maandalizi yake hayo, mara ya mwisho  Stars ilikwaana na Zambia Desembza 22 mwaka jana kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na  kuibanjua bao 1-0 katika mchezo wa kirafiki .

Comments