YONDAN, DOMAYO KUUNGANA NA STARS ETHIOPIA


KIKOSI cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kimeondoka jana alasiri kwenda Addis Ababa, Ethiopia  bila ya nyota wa Yanga, Kelvin Yondan na Frank Domayo ambao walitakiwa kujiunga na timu hiyo juzi usiku wakitokea nchini Uturuki. 
Kikosi cha Stars kinakwenda Ethiopia kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya wenyeji utakaopigwa kesho katika dimba la Taifa la Addis Ababa. 
Awali, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia kwa Ofisa Habari wake, Boniface Wambura alisema juzi  kwamba wachezaji hao wangutua nchini juzi usiku na kuambatana na wenzao katika safari ya jana. 
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, kabla ya kuondoka kwenda Ethiopia, Meneja wa Stars Leopard Mukebezi alisema kwamba wachezaji hao wataungana na wenzao Ethiopia baada ya kushindwa kutua juzi. 
Alisema mbali na wachezaji hao, wachezaji wengineo ambao hawatakuwemo kwenye kikosi hicho ni pamoja na Athuman Idd I ‘Chuji’ Simon Msuva na Nadir Haroub ‘Canavaro’ ambao wapo Ututruki na klabu yao ya  Yanga, Mwadini Ally ambaye amebaki na timu yake ya Azam inayoshiriki kombe la Mapinduzi, pamoja na John Bocco ambaye yupo nchini India kwa matibabu. 
Wachezaji ambao wamekwenda huko ni pamoja na Makipa Juma Kaseja (Simba) ambaye ndiye nahodha na  Aishi Manula (Azam FC), wakati Mabeki ni Aggrey Morris, Issa Rashid, Erasto Nyoni (Azam), Amir Maftah na Shomari Kapombe (Simba). 
Viungo ni Salum Abubakar, Khamis Mcha (Azam), Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto (Simba), na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar).
Washambuliaji ni Mbwana Samata, Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo- DRC), na Mrisho Ngasa (Simba). 
Mchezo kati ya Stars na Ethiopia ni maandalizi ya mwisho Ethiopia kabla ya kwenda Afrika Kusini kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), zitakazoanza Januari 19 mwaka huu.
Aidha, Stars  itautumia mchezo huo kama sehemu ya maandalizi ya mechi ya mchujo dhidi ya Morocco kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia 2014, mchezo utakaochezwa Machi mwaka huu. 
Katika maandalizi yake hayo, mara ya mwisho Stars ilicheza na Zambia ‘Chipolopolo’ Desemba 22 mwaka jana kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kuibanjua bao 1-0.