YANGA WAMKOSA KABANGE TWITE


WAKATI  Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa ikimwidhinisha kipa Shaban Kado kuidakia Coastal Union ya Tanga, Yanga watamkosa kiungo Kabange Twite katika raundi ya pili ya Ligi Kuu itakayoanza Jumamosi hii.
Kabange  ambaye ni pacha wa beki wa Mbuyu Twite katika kikosi cha Yanga,   alisajiliwa Januari kutoka FC Lupopo ya DR Congo, lakini hayumo kwenye orodha ya nyota waliosajiliwa dirisha dogo la usajili iliyotolewa jana na TFF.
Awali, TFF ilimzuia Kabange Twite kuichezea Yanga hadi pale suala lake litakapoamuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), baada ya Yanga kushindwa kupata idhini ya FC Lupopo ya kumsajili nyota huyo, hivyo Fifa ndio walipasa kutoa idhini.
Viongozi wa Yanga kwa upande wao waliwasiliano na Lupopo kwa njia ya Kompyuta (TMS) masaa mawili kabla ya usajili wa dirisha dogo kufungwa Desemba 15, lakini hawakupata majibu, hivyo suala hilo kuendelea kubaki mikononi mwa Fifa chini ya Kamati ya Haki na Uhamisho Wachezaji.