YANGA KUCHEZA MECHI YA MWISHO LEO UTURUKI
Wachezaj wa Young Africans wakifanya mazoezi jana  asubuhi kujiandaa na mchezo wa leo dhidi ya Emmen FC ya Uholanzi
Timu ya Young Africans Sports  Club leo itashuka dimbani kucheza mchezo wake wa mwisho na watatu (3) dhidi ya  timu ya Emmen FC ya ligi daraja la kwanza nchini Uholanzi  katika mchezo wa kirafiki utakaofanyika katika viwanja vya Adora football - Berek pembeni kidogo ya mji wa Antlaya.

Young Africans ambayo imeshakaa takribani siku 12 katika mji wa Antalya na kucheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya timu za Armini Bielefeld ya Ujerumani na Denizlispor ya Uturuki leo asubuhi imeendelea na mazoezi katika viwanja vya Fame Residence football mjini Antalya. 
Kocha Mkuu wa Young Africans Ernest Brandts amesema atatumia mchezo huo wa mwisho kama fursa pekee kwao kwani mchezo huo utakuwa kipimo kizuri kwao kwani timu ya Emmen FC ni timu nzuri na ndio maana ipo katika ligi daraja la kwanza nchini Uholanzi.
Akiongelea mchezo huo wa kesho  Brandts amesema timu ya Emmen FC ni timu nzuri, imekuja Antalya kuweka kambi ya mafunzo kujiandaa na mzunguko wa ligi daraja la kwanza nchini Uholanzi, hivyo ni nafasi nzuri ya kujipima uwezo na timu hiyo ya Uholanzi.
Aidha wachezaji Frank Domayo na Kelvin Yondani waliokuwa wameondoka jana jioni kuelekea nchini Ethiopia wameshindwa kuungana na wachezaji wenzao wa timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars baada ya jana jioni kufika Istambul  kukuta tiketi zao za kwenda Addis Ababa ni za tarehe 09 Februari 2013  hali iliyopelekea kukwama Istambul na kuamua kurejea mjini Antalya kuungana na wachezaji wenzao waliopo kambi.
Kikosi cha wachezaji 27 waliopo kambi mjini Antalya kimeendelea na mazoezi ya asubuhi kujiandaa na mchezo huo wa kesho amabao utakua ni mchezo wa mwisho kabla ya timu ya Young Africans kuanza safari ya kurejea nchini Tanzania siku ya jumapili.
Young Africans inatarajia kuondoka mjini Antalya siku ya jumapili mchana kupitia Istambul ambapo itaondoka majira ya saa 1 usiku, saa 2 usiku kwa saa za Afrika Mashariki na inatarajiwa kufika Dar es salaam Tanzania majira ya saa 10 usiku kasoro.

Jerson Tegete, Omega Seme & Ladislaus Mobgo wakiwa mazoezini leo asubuhi