UCHAGUZI MKUU TAFCA WAPIGWA KALENDA


Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeahirisha uchaguzi wa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) uliokuwa ufanyike leo (Januari 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam. 
Uchaguzi umeahirishwa kwa vile ulitaka kufanyika bila kuzingatia Katiba ya TAFCA Ibara ya 32(1) na Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF Ibara ya 10(6) na 26(2), hivyo Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeahirisha uchaguzi huo kwa vile nafasi zilizoombwa kugombewa na idadi ya waombaji uongozi haikidhi matakwa ya Katiba ya TAFCA. 
Pia taratibu za kikanuni ikiwa ni pamoja na kuwaarifu waombaji uongozi ambao hawakukidhi matakwa ya Katiba ya TAFCA hazikukamilika kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF. 
Licha ya upungufu huo, TAFCA haikuwasilisha taarifa za mchakato mzima kama ilivyoombwa na TFF. Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeiagiza Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA kuandaa uchaguzi mpya utakaokidhi matakwa ya Kamati ya TAFCA baada ya Uchaguzi Mkuu wa TFF.

TFF inaishauri TAFCA kutumia fursa ya Mkutano Mkuu wa leo (Januari 19 mwaka huu) kujadili mustakabali wa TAFCA kwa kuwa chama hicho kimeshindwa mara mbili kupata idadi ya wagombea wanaokidhi akidi ya Kamati ya Utendaji.

Pia TAFCA haijawahi kufanya mikutano ya Kamati ya Utendaji na Mkutano Mkuu kwa karibu miaka minne.


Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Comments