TEGETE AIFUTA MACHOZI YANGA UTURUKI

YANGA SC imefungwa mabao 2-1 jioni ya jana  na Denizlispor FC ya Denizli, nchini Uturuki katika mchezo wake wa pili wa kujipima nguvu katika ziara yake ya Uturuki, bao la kufutia machozi likifungwa na Jerry Tegete.
Pamoja na kufungwa na timu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, iitwayo Bank Asya 1. Lig, ambayo msimu uliopita ilimaliza katika nafasi ya 10, Yanga ilicheza soka ya kuvutia.
Denizlispor Football iliyoanzishwa mwaka 1966, inatumia Uwanja wenye kuingiza mashabiki 19,500 wa Denzili Ataturk na mafanikio yake makubwa hivi karibuni ilikuwa mwaka 2002 waliposhika nafasi ya tano katika Ligi Kuu ya nchini humo na kufuzu kwenye mchujo wa Kombe la UEFA.
Mwaka huo, ilifanya maajabu kwa kuzifunga timu zenye majina Ulaya kama FC Lorient, Sparta Prague na Olympique Lyonnais, kabla ya kufungwa katika Raundi ya Nne na FC Porto ya Ureno, ambao walitwaa ubingwa wa michuano hiyo mwishowe.
Katika mchezo wake wa kwanza wa kujipima nguvu, Yanga ilitoka 1-1 na DSC Arminia Bielefeld ya Ujerumani, bao la timu hiyo ya Jangwani likifungwa na Tegete.
Kikosi cha Yanga leo kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdu, Kabange Twite, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Athumani Iddi ‘Chuji’, Haruna Niyonzima, Nurdin Bakari, Jerry Tegete/Didier Kavumbangu, Said Bahanuzi/Hamisi Kiiza na Simon Msuva.

Comments