TAMASHA LA USIKU WA MASTAA WA FILAMU LAIVA





Mwenyekiti wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) Simon Mwakifamba akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tamasha la kukusanya fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya ofisi zao Kulia ni msanii Mrisho Mpoto na Suzan Lewis 'Natasha'.

WASANII wa muziki wa kizazi kipya wakiwemo Harid Tunda ‘Tundaman’,  Seleman Msindi ‘Afande Sele’, Mrisho Mpoto ‘Mjomba’  na Vitalis Maembe wamejitosa kutoa burudani katika tamasha la ‘Usiku wa Mastaa wa Filamu’ litakalofanyika keshokutwa  kwenye ukumbi wa Dar Live, Mbagala jijini Dar es Salaam. 
Tamasha hilo lenye lengo la kukusanya kiasi cha sh milioni 60 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya ofisi za Shirikisho la filamu Tanzania (TAFF), limeandaliwa na TAFF kwa kushirikiana na Vannedrick Tanzania Limited. 
Mwenyekiti wa TAFF Simon Mwakifambwa alisema maandalizi kwa ajili ya tamasha hilo yamekamilika, hivyo amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi. 
Alisema wameamua kusaka fedha hizo ili kuweza kupatikana kwa vitendea kazi na fenicha ambazo zitaendana na hali halisi ya sasa, pia kuwezesha watendaji wa shirikisho hilo. 
Aliongeza kuwa, usiku huo ambao utatawaliwa na burudani zaidi, mbali na wasanii hao wa bongo fleva, pia wasanii wa filamu wanaoimba muziki wakiwemo Shilole, Hemed PHD, Masanja Mkandamizaji, Bingwa wa Rivas Alex Macheje, Kitale, Snura na Jini Kabula. 
“Pia tutakuwa na bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’Joti, The Super Star King  Majuto  Shija, Mtunis, Rado, Dude, Mangi, Matata, Kingwendu na wengineo’, alisema 
Aidha, kutakuwa na shoo ya sebene kutoka kwa kundi la Bongo Muvi Unity likiongozwa na JB, Ray, Irene Uwoya, Jackline Wolper,Wema Sepetu, Steve Nyerere, Dk.Cheni, Mr.Chuz na Yobnesh ‘Batuli’ na wengine wengi. 
Usiku huo ambao kiingilio ni sh.7,000 , 15,000 kwa VIP na sh.2,000 kwa watoto umedhaminiwa na DTV, Global Publishers, Lamada Hotel, Times Fm, Umoja Drink, Clouds Media na Vannedrick Tanzania Limited.

Comments