STARS KUIKWAA ETHIOPIA LEO BILA YONDAN, DOMAYO


TIMU ya Soka ya Tanzania, Taifa Stars leo inatarajiwa kushuka dimbani kukwaana na wenyeji wao Ethiopia bila nyota wake Kelvin Yondani na Frank Domayo ambao wameshindwa kuungana na wenzao wakitokea nchini Uturuki.
Nyota hao waliopo na timu yao ya Yanga nchini Uturuki walikokwenda kwa kambi kujiandaa na
Raundi ya pili ya Ligi Kuu Bara, walipaswa kuungana na Stars nchini Ethiopia jana, baada ya awali kushindwa kujiunga nao jijini Dar es Salaam.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Abdallah Binkleb, alisema jana kwamba, nyota hao wameshindwa kuungana na wenzao Ethiopia, kutokana na makosa yaliyofanywa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), katika kupanga safari yao.
Alisema, nyota hao ambao walitokea Antalya Uturuki walipopiga kambi na wenzao, walijikuta wakikwama jijini Istanbul kutokana na kasoro hizo, hivyo uongozi wa Yanga kulazimika kuingia gharama za kuwarejesha Antalya tena.
Awali, Yanga ilitoa ruhusa kwa wachezaji hao wawili kati ya watano walioitwa Stars kwa ajili ya mchezo huo huku TFF ikidai wangeungana na wenzao Ethiopia.
Mchezo wa leo ambao ni  kirafiki, utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Addis Ababa, ambako Stars ilitua salama Ethiopia juzi  na kufikia kwenye hoteli ya Hilton.
Mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 11:30 jioni,
ni muhimu kwa timu zote kwani wakati Ethiopia kama kipimo kuelekea fainali za Afrika, Stars inajipanga kwa mechi ya kuwa nafasi ya fainali
za Kombe la Dunia dhidi ya Morocco.
Fainali hizo za 29, zimepangwa kufanyika nchini Afrika Kusini kuanzia Januari 19 hadi Februari 10, mwaka huu.
Akizungumzia mchezo huo kabla ya kuondoka, Kocha Mkuu wa Stars, Kim Poulsen alisema, licha
ya kuwa ni mchezo wa kirafiki, unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, kwani ushindi utaongeza hamasa.
Alisema kuwa, mchezo huo pia utakuwa na manufaa kwa Stars, kwani ni sehemu ya maandalizi ya mechi dhidi ya Morocco, ambayo ni ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia 2014, mechi itakayopigwa Machi mwaka huu.
“Nashukuru kwa kupata mechi hii, ambayo pia itatusaidia na sisi katika maandalizi yetu dhidi ya Morocco, ni yangu matumaini vijana watatimiza wajibu wao,” alisema.
Poulsen aliongeza kuwa, mchezo wa leo utasaidia kumpa mwanga wa kikosi chake hicho ili kuweza kukifanyia marekebisho pindi watakaporejea nchini.
Katika maandalizi yake hayo, mara ya mwisho Stars ilicheza na Zambia ‘Chipolopolo’ Desemba 22 mwaka jana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kuibuka na ushindi wa mabao 1-0.
Kikosi cha Stars kinaundwa na makipa Juma Kaseja (Simba), ambaye ndiye nahodha na Aishi Manula (Azam FC), wakati mabeki ni Aggrey Morris, Issa Rashid, Erasto Nyoni (Azam), Amir Maftah na Shomari Kapombe (Simba).
Viungo ni Salum Abubakar, Khamis Mcha (Azam), Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto (Simba), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), huku washambuliaji ni Mbwana Samata, Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo- DRC), na Mrisho Ngasa (Simba).