SOKA YA VIJANA WAANZISHA UMOJA MOROGORO


Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Vilabu vya soka ya vijana, watoto na wanawake katika Manispaa ya Morogoro vimeanzisha umoja wao kwa lengo la kujipatia mafanikio zaidi katika mchezo huo. 
Uamuzi wa kuunda umoja huo ulifikiwa wikiendi iliyopita katika mkutano wa viongozi wa vilabu hivyo uliofanyika katika ukumbi wa DDC, mjini hapa. 
Viongozi wa muda waliochaguliwa kuongoza umoja huo na nafasi zao zikiwa katika mabano ni Tike Tike Dimoso (mwenyekiti), Patrick Fulano (makamu mwenyekiti), Gasper Mashenene (katibu mkuu), Adam Costantino (mweka hazina), Daudi Julian  (mratibu) na Juma Mgonja (mjumbe).  
Akizungumza mara baada ya uchaguzi huo, mwenyekiti wa Umoja huo, Dimoso alisema lengo ni kuhakikisha vilabu vya soka ya vijana, watoto na wanawake katika manispaa ya Morogoro vinapiga hatua kubwa katika mchezo huo na hivyo kujiweka katika mazingira mazuri ya kuibua vipaji zaidi vya wanasoka chipukizi. 
Dimoso alisema uongozi wa Umoja huo tayari umeshaanza kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuandaa rasimu ya katiba. 
“Huu ni umoja wa aina yake na ni wa kwanza kuanzishwa katika manispaa ya Morogoro na mkoa kiujumla hivyo naamini tutafanikiwa”, alisema. 
Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa wadau wa soka mkoani Morogoro kuusaidia Umoja huo kwa hali na mali ili kuhakikisha unatimiza malengo yake. 
Vilabu vilivyokutana na kuasisi Umoja huo ni Al Futuh United, Young Boys, Jamhuri Boys, CIDA Kids, Mazimbu FC, Mwere Kids, New Kids na Kingo Kids.

Comments