SIMBA SC WAPAA UMANGANI LEO


MABINGWA wa Bara, Simba SC wanatarajiwa kuondoka leo Dar es Salaam kwenda Oman kuweka kambi ya wiki mbili kujiandaa na Ligi Kuu pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kuhusu Kombe la Mapinduzi, Simba imegawa vikosi viwili na kile ambacho kilichukua Kombe la Sup8R Banc ABC kwa kuzifunga Azam FC na Mtibwa Sugar ndicho kitabaki kwenye Kombe la Mapinduzi chini ya kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na Mganda Richard Hamatre.
Kikosi hicho cha Mapinduzi kina wakali kama Ramadhan Singano ‘Messi’, Edward Christopher, Abdallah Seseme, Haruna Chanongo, Hassan Isihaka, Hassan Hatibu, Miraj Adam na wengine ambao wote wanachezea Simba A.
Wachezaji wanaobaki kwenye Kombe la Mapinduzi, watakwenda Oman baada ya mashindano hayo pamoja na kocha Julio.
Simba SC kesho inatarajiwa kumenyana na Azam FC katika Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Mchezo huo utakuwa ni marudio ya Nusu Fainali ya mwaka jana, ambayo Azam FC waliitoa Simba SC kwa kuichapa mabao 2-1.
Kocha Msaidizi wa Azam FC, Muingereza Kalimangonga Sam Daniel Ongala, maarufu kama Kali, amesema kwamba wamefurahia kukutana na Simba SC katika Nusu Fainali kuliko Tusker ya Kenya, kwa sababu hiyo itakuwa njia ya mkato kwao kuingia Fainali.
Ikiwa Oman, Simba itakaa kwa wiki mbili na itacheza mechi tatu za kujipima nguvu dhidi ya timu ambazo wameandaliwa na wenyeji wao Fanja FC. Aidha, wameandaliwa makocha watatu huko, wakiongozwa na beki wa zamani wa Simba SC, Talib Hilal kuungana na makocha wa Simba kuinoa klabu hiyo ikiwa nchini humo.
Hiyo ni ziara ya mafunzo, ambayo lengo lake ni kuiweka sawa Simba SC kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.