SAFARI YA SIMBA OMAN YANUKIA, TAYARI PASIPOTI ZA WACHEZAJI ZATUMWA


UONGOZI wa klabu ya Simba umepeleka hati za kusafiria za wachezaji wake nchini Oman ili kuweza kupatiwa vibali vitakavyowaruhusu kuingia nchini humo. 
Simba ambayo kwa sasa ipo Visiwani Zanzibar ikishiriki michuano ya kombe la Mapinduzi, awali ilipanga kwenda Oman kesho kwa ajili ya kambi maalum ya kujiandaa na ligi kuu ya Vodacom na michuano ya kimataifa. 
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, Mwenyekiti wa Simba Alhaj Ismail Aden Rage alisema jana kwamba wamelazimika kuzitumna hati hizo Oman kutokana na utaratibu wa sasa unavyohitajika. 
“Viza zote za kuingia nchini Oman kwa sasa zinatakiwa kuomba hukohuko kwao hivyo  tumemetuma hati za kusafiria za wachezaji na viongozi watakaokwenda na baada ya hapo tutapanga safari,”alisema 
Alisema mara baada ya kupatiwa viza ndipo wataamua rasmi ni lini watakwenda huko lakini wanatarajia safari yao itakuwa kuanzia Januari 10 mwaka huu,huku pia wakiangalia mwenendo wa timu yao katika kombe la Mapinduzi. 
Rage aliongeza kuwa iwapo watafanikiwa kwenda Oman, pamoja na mazoezi ya kawaida pia watacheza michezo kadhaa ya kujipima nguvu na timu za huko ikiwemo Fanja Fc. 
Mabingwa hao watetezi wa ligi kuu ya Vodacom walimaliza mzunguko wa kwanza na kushika nafasi ya tatu nyuma ya Azam Fc na Yanga iliyoshika nafasi ya kwanza, hivyo uongozi uliamua kuipeleka nje ya nchi kwa ajili ya kuweka kambi. 
Aidha, mabingwa hao wataanza kampeni yao katika klabu bingwa Afrika kwa kucheza na Recreativo de Libolo ya Angola kati ya Februari 17 na 19 kwa kucheza nyumbani.