POULSEN ATUA BONDENI KUZIDODOSA IVORY COAST NA MOROCCO


Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen (pichani) ameondoka leo mchana (Januari 18 mwaka huu) kwa ndege ya South African Airways kwenda Afrika Kusini kuzifuatilia timu za Ivory Coast na Morocco zinazoshiriki Fainali za 29 za Mataifa ya Afrika (AFCON) zinazoanza kesho (Januari 19 mwaka huu) nchini humo. 
Ivory Coast na Morocco ziko kundi moja na Tanzania (Taifa Stars) katika kinyang’anyiro cha kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil. 
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, na inayoshika nafasi ya pili katika kundi hilo ambalo pia lina timu ya Gambia itacheza na Morocco, Machi 24 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.