OKWI ATUA SAHEL KWA DOLA 300,000

MSHAMBULIAJI wa Simba SC, Mganda Emmanuel Okwi ameuzwa klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia kwa dola za Kimarekani 300,000.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe ameiambia SPORTS LADY mida hii kwamba, Okwi amekamilisha vipimo na kila kitu na tayari amesaini mkataba.
“Tunasubiri kulipwa fedha zetu tu, viongozi watakwenda Tunisia kuchukua fedha za mauzo ya mchezaji huyo,”alisema Poppe.
Okwi amekuwa akipiga chenga kuripoti kambini Simba SC na alikuwa hata hapokei simu za viongozi wa klabu hiyo kila alipopigiwa.
Kufuatia hatua hiyo, uongozi ulimuengua kwenye programu ya safari ya Oman na sasa inabainika ametua Sahel.
Okwi, aliyezaliwa Desemba 25, mwaka 1992 aliisajiliwa Simba akitoea SC Villa ya Uganda mwaka 2010 akiwa kinda wa miaka 17, akisajiliwa kwa dau la dola za Kimarekani 40,000.
Baada ya kumaliza mkataba wake wa awali, Desemba mwaka jana aliongeza mkataba wa miaka miwili na Simba SC ambao kabla hajaanza kuutumikia, anahamia Sahel.

Comments