MAHABUSU KUMPONZA HASSANOO UCHAGUZI WA TFF


NAFASI ya Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa Pwani (COREFA), Hassan Othman ‘Hassanoo’ kugombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imeota mbawa.
Hassanoo ambaye yupo mahabusu akikabiliwa na mashitaka ya kudaiwa kuhujumu uchumi na wizi wa shaba, aliomba kuwania nafasi hiyo kupitia Kanda namba 11, inayowakilisha Mikoa ya Morogoro na Pwani, alichukuliwa fomu na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Corefa, Masau Bwire.
Hata hivyo, kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa TFF, itamuwia vigumu Hassanoo kushiriki usaili uliopangwa kufanyika Februari 1 hadi 4 kutokana kuwa mahabusu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Deogratius Lyato, akizungumzia hilo, alijibu kwa kifupi na kuwa, lazima mgombea ahudhurie usaili mwenyewe na si kutuma mwakilishi.
 “Sisi tutapeleka barua za kumtaka kila mgombea afike kwenye usaili, kinyume na hapo kanuni zipo wazi,” alisema.