KAMPUNI TANO ZAOMBA TENDA UKARABATI TFF


Kampuni tano zimewasilisha tenda zao kuomba kupewa kazi ya kukarabati hosteli ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Januari 7 mwaka huu TFF ilitangaza tenda kwa ajili ya ukarabati wa hosteli hiyo baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kukubali ombi lake la kutoa fedha kwa ajili ya kazi hiyo. 
Ufunguzi wa tenda hizo ulifanyika jana (Januari 28 mwaka huu) kupitia kwa Bodi ya Tenda ya TFF mbele ya wazabuni wote watano waliowasilisha tenda zao na kushuhudiwa pia na Mkandarasi mshauri. Wazabuni (kampuni) waliojitokeza awali walikuwa saba, lakini waliorejesha zabuni zao ni watano. 
Kampuni hizo ni Crescent Concrete Limited, DGS Company Limited, Mart Builders Company Limited, Prince General Investment Limited na Send Star Company Limited. 
Bodi ya Tenda ya TFF itakutana Januari 31 mwaka huu pamoja na mambo mengine kuchagua kampuni ambayo itafanya ukarabati huo.