KABURU:NIMEJITOA TFF KUWAACHIA MABOSI ZANGU

MAKAMU mwenyekiti wa Simba Geofrey Nyange 'Kaburu' (Pichani)amesema ameamua kutorudisha  fomu za kuwania  ujumbe wa kamati ya utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia kanda ya Morogoro na Pwani ili kuwapisha 'Mabosi' wake ambao pia wamejitosa katika uchaguzi huo.
Kaburu ambaye pia ni mjumbe wa mkutano mkuu wa TFF akiwakilisha mkoa wa Pwani, katika uchaguzi huo aliomba nafasi hiyo sambamba na mwenyekiti wa chama cha soka Mkoa wa Pwani (COREFA), Hassan Hassanoo na Katibu wa COREFA, Riziki Majala.
Kaburu ameiambia Sports Lady leo  kwamba kwa hali hiyo asingeweza kushindana na wakubwa zake hivyo ameamua kuwapa nafasi  hiyo muhimu.
"Mtu kama umelelewa kwa miongozo mizuri huna budi kuheshimu wakubwa zako, hivyo baada ya kuona wakubwa zangu nao wamechuakua fomu niliona si busara kuendelea na uchaguzi tena,"alisema.
Mbali na Hassanoo na Majala, wengine waliojitosa ni Farid Nahdi na Twahir Njoki ambapo uchaguzi wa TFF unatarajiwa kufanyika Februari 24 jijini Dar es Salaam.