FUNGU LA PILI WACHEZAJI SIMBA KUONDOKA LEO


FUNGU la pili la wachezaji wa klabu ya Simba, linatarajiwa kuondoka jijini leo jioni kwenda Oman kuungana na wenzao walioweka kambi kwa ajili ya kujiwinda na Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa.
Awali, fungu la kwanza likiongozwa na Kocha Mkuu Patrick Liewing na Meneja wa timu, Moses Basena liliondoka juzi kwenda huko kwa ajili ya kambi hiyo maalum ya maandalizi.
Kocha Msaidizi, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ambaye alibaki na kundi la pili kwa ajili ya mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi linaloendelea visiwani Zanzibar, kabla ya kutolewa na Azam Fc juzi usiku, ndiye atakayeongoza msafara huo.
Julio, aliwataja wachezaji watakaoondoka leo kuwa ni pamoja na William Mweta, Miraji Adam, Paul Ngalema, Hassan Isihaka, Komabil Keita, Jonas Mkude, Ramadhan Singano ‘Messi’, Abdallah Seseme na Said Demla.
Kundi jingine la wachezaji wa Simba, litahusisha waliopo timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ambayo ipo nchini Ethiopia, ambao wataungana na wenzao kesho.
Simba ambayo itaiwakilisha Tanzania katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, itaanza kwa kucheza na Recreativo do Libolo ya Angola kati ya  Februari 17 na 19 jijini Dar es Salaam.