ESPERANCE, ETOILE DU SAHEL ZAMKANA OKWI

WAKATI klabu  za Esperance  na Etoile du Sahel za Tunisi zikimkana mshambuliaji wa Simba Emmanuel Okwi, imebainika kwamba nyota huyo yupo nchini kwao Uganda.
Hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari nchini vilimkariri Mwenyekiti wa Simba Alhaj Ismail Aden Rage akisema kwamba nyota huyo ameshindwa kujiunga na wenzake kutokana na kuwa nchini Tunisia akifanya majaribio katika klabu ya Esperance.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umethibitisha kwamba nyota huyo ambaye amekuwa akiiumiza sana kichwa klabu yake ya Simba hayupo nchini humo kama ilivyoripotiwa.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Rage alizikana taarifa za Okwi kujaribiwa Esperance na kudai kwamba anajaribiwa Etoile Du Sahel.
“Okwi hayupo Esperance bali ni Etoile Du Sahel…anaendelea na majaribio yake na kama kutakuwa na taarifa zozote mtaarifiwa,”alisema
Hata hivyo, mwandishi wa habari hizi aliwasiliana na Mwenyekiti wa Etoille Ridha Charfeddine ambaye alikana kuwepo kwa mchezaji huyo anayefanya majiribio katika timu yao.
“Hatuna mchezaji anayeitwa Okwi kwenye timu yetu…pia hatuna mchezaji yoyote kutoka Uganda ambaye tunamfanyia majaribio,”alisema
Tanzania Daima Jumapili lilipomtafuta tena Rage ili kujua ukweli wa taarifa hizo halikufanikiwa kumpata baada ya simu zake kutokuwa hewani.
Okwi ambaye mwioshoni mwa mwaka uliopita alisaini mkataba mpya wa kuitumikia Simba, amekuwa na tabia ya kuumiza vichwa vya viongozi wa timu hiyo pindi anapoenda likizo kwao kwa kushindwa kurejea nchini kwa wakati anaotakiwa.
Rage pamoja na mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hanspoppe walimfuata Okwi kwa Uganda alipokuwa akiitumikia timu yake ya Taifa ‘The Cranes’ katika michuano ya Chalenji na kumsainisha mkataba mpya.
Hali hiyo imepelekea uongozi kumfuta katika safari ya Oman ambapo Simba ipo huko kwa kambi maalum ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Vodacom pamoja na michuano ya kimataifa ambapo itashiriki klabu bingwa ya Afrika itakapoanza kampeni kwa kucheza na  Recreativo do Libolo ya Angola kati ya  Februari 17 na 19 jijini Dar es Salaam.
Hii ni mara nyingine tena ya kuyibuka kwa utata wa mchezaji huyo kujaribiwa nje baada ya mwezi Julai mwaka jana kudaiwa kufanya majaribio katika klabu ya Redbull Salzburg ya Austria huku viongozi wakitoa taarifa za kujichanganya.
Viongozi hao walidai Okwi kufuzu majaribio hayo na hivyo wangemuuza kwa Euro  600,000 (sawa na Sh. bilioni 1.1), kabla ya baadaye nyota huyo kukana kufanya majaribio katika klabu hiyo.
Okwi aliweka wazi kwamba hakuwahi kufanya majaribio hata siku moja nchini Austria kwani tangu alipotua huko alikuwa mgonjwa hivyo kutokana na kuugua, uongozi ulimtaka arejee nyumbani na hadi atakapoitwa tena.
Katika hatua nyingine, Simba inatarajiwa kucheza mchezo wake wa kwanza keshokutwa dhidi ya  Olimpiki ya Oman, kabla ya Januari 18 kuikabili Suwqi  na baadaye kupiamana ubavu na  Fanja FC.