DARAJA LA KWANZA FEB 2, SMALL KIDS YASHUSHWA DARAJA


Wakati mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara unaanza Jumamosi (Januari 22 mwaka huu), mzunguko wa pili wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) umesogezwa mbele kwa wiki moja ambapo sasa utaanza Februari 2 mwaka huu.

Uamuzi wa VPL kuendelea Januari 26 mwaka huu ulifikiwa katika kikao cha Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na klabu za ligi hiyo kilichofanyika jana (Januari 21 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, uamuzi huo umefikiwa huku yakiwepo masharti kadhaa kutokana na uamuzi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukamata sh. milioni 157 kwenye akaunti za TFF, fedha ambazo zilitoka kwa mdhamini wa VPL (Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom) kwa ajili ya timu zinazoshiriki ligi hiyo.

Masharti hayo yatawasilishwa na Kamati ya Ligi kwa maandishi kwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), nakala kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo. Awali klabu kupitia Kamati ya Ligi zilisisitiza zisingecheza ligi hadi fedha hizo zitakaporejeshwa.

Kwa upande wa FDL itaanza bila timu ya Small Kids ya Rukwa ambayo imeshushwa daraja kwa mujibu wa kanuni baada ya kushindwa kucheza mechi mbili katika mzunguko wa kwanza.

Kwa mujibu wa kanuni za ligi hiyo, matokeo yote ya mechi ambazo Small Kids ilicheza katika mzunguko huo wa kwanza yamefutwa. 

Comments